Articles

WAJIBIKA KUTATUA JANGA LA TAKA JIJINI

BY CAROLINE BOYANI OYARO

Miongoni mwa kaunti arobaini na saba za Kenya, Nairobi ndiyo inayoongoza kwa idadi ya wakaazi kulingana na sensa iliyofanyika mwaka wa elfu mbili na kumi na tisa. Hata hivyo, Nairobi kama vile miji mingine mikubwa inakumbwa na janga la kutupa ovyo na kutohifadhi taka kinyume na inavyostahili. Serikali ya kaunti hiyo inadai kuweka mikakati mbadala ili kushughulikia suala hili ila wakaazi wa mji huo watalazimika kungoja sana kabla ya mambo kubadili mkondo kwa njia hiyo inayotakikana.

Nairobi ni nyumbani mwa mitaa ya mabanda ikiwemo Korogocho, Mukuru kwa Njenga, Kibera miongoni mwa mengine. Baadhi ya maeneo katika mitaa hii yamejawa na biwi la taka zilizotapakaa ovyo ovyo. Utawapata watoto wadogo wakichezea papo hapo huku wakitia vidole midomoni mwao bila kutahadhari. Wazazi wengi wamesikika wakilalamika haswa wakati wa likizo ndefu. Mkaazi mmoja wa maeneo ya Viwandani, Bi. Maria, alilalamikia utepetevu wa viongozi wa kijiji hicho, “Hapo awali tulikua tunakusanya taka wiki nzima kisha kila jumamosi vijana wa mtaa wanapita wakichukua kwa ada ndogo ila baadhi ya viongozi hawakuwalipa na hivyo mradi huo ukasitishwa ghafla.” alisema Bi. Maria akiongezea kuwa ukosefu wa ushirikiano baina ya wakazi na viongozi hao unachangia kutokua kwa mikakati ya kuyalinda mazingira.

Wengi wa watu wanaoishi katika mitaa hiyo ni wa kipato cha chini na nyumba zao zimerundikana. Bwana Yohana anayeishi katika mtaa wa Mukuru kwa Njenga alisisitiza kuwa hatua ya haraka inafaa kuchukuliwa ili kuwezesha kudhibiti hali hii. “Mabomba ya maji yamepitishwa kwenye mitaro michafu licha ya kuwa maji yayo hayo ndiyo yanatunatumika katika kupika na pia kunywa.” Alisema Bwana Yohana. Hali hii inahuzunisha sana haswa mvua inaponyesha na mitaro hio kujaa kupita kiasi. Maji hayo machafu hupata nafasi ya kuingia katika nyumba za watu na kuzua hofu kama si kuwakosesha amani.

Eneo kama Viwandani lililo na viwanda vingi liimehadhirika zaidi. Kampuni mbalimbali humimina taka na kemikali hatari kwenye mto Nairobi unaotenganisha mtaa wa Viwandani na Mukuru kwa Reuben, wakaazi nao wanatilia chumvi kwa kidonda kwa kujaza taka kwenye kingo za mto huo. Ingekuwa kwamba kila mja anawajibika katika hiyo kaunti ya, Nairobi ingepiga hatua kubwa na kuwekeza raslimali katika miradi mingine ili kuwanufaisha wenyeji wa mji huo na hata nchi nzima kwa ujumla.

Iwapo serikali ya kaunti hiyo haitaungana na viongozi wa mitaa tofauti tofauti katika kutetengeneza mabomba ya kupitisha maji machafu kando ya barabara, basi jambo hilo laweza kuwa sugu zaidi. Mabomba haya yanaweza kufananishwa na hali ya kuficha kidonda ambacho baadae kitaoza na kuzaa maradhi yasiyokuwa na tiba. Mabomba haya hayapitishi maji inavyostahili na kwa muda mfupi huzibwa kutokana na taka inayojilimbikiza. Mvua inaponyesha, mabomba haya huwa yanashindwa kustahimili shinikizo la maji mengi na hili hupelekea barabara kufurika na kisa kuwazuwia watu kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Matatizo haya yametokea sana sana baada ya watu kutotia maanani kanuni za kulinda mazingira. Baadhi ya wakaazi wa mitaa hii hutupa hata choo barabarani. Wengine wamepita mipaka hata kuweka taka nje ya majumba ya kusali kama vile misikiti na makanisa. Mtu aliye na akili zake timamu bado ataona ukuta umeandikwa usitupe taka hapa ovyo miongoni mwa onyo zinginezo na bado mtu huyo huyo atajitia hamnazo na kuwacha taka hapo. Jua linapowaka huzichoma taka hizo na kuleta harufu inayochafua hewa. Kunadhifisha mazingira huleta mandhari mazuri na hewa safi.

Serikali ina wajibu wa kubuni mbinu zifaazo kuleta hali ya uchafuzi wa mazingira kikomo. Wale watakao patikana wakitupa taka ovyo wapewe adhabu kali ili iwe funzo kwa wengine wenye tabia kama hizo, kwani tabia nzuri ni mazoea na vile vile tabia mbaya ni mazoea. Kando na kufungwa jela au kupigwa faini, wanafaa waamrishwe kusafisha uchafu wote kutoka mitaa hiyo. Vilevile serikali inaweza kuwateua vijana watakao shughulikia ukusanyaji wa taka kisha zihifadhiwe vyema au kuchomwa katika sehemu fulani.

Ni mwito kwa kila mtu kuungana katika kunadhifisha mazingara ya kaunti ya Nairobi. Kila mtu akijuhumuika hapatakuwa na haja ya askari wa kaunti kusumbuana na wakaazi. Kawaida tutilie maanani kuwa asili ina njia kali ya kutuadhibu iwapo hatutahadhari kabla ya hatari.

Related posts
Articles

Digital Activism and the Youth Bravado (Millennials and Gen Z)

Articles

SHOULD WE ADOPT STRATEGIC AMBIGUITY AS FOREIGN POLICY?

Articles

KENYA’S FINANCE BILL 2024, IN A NUTSHELL

Articles

Mwizi! Mwizi! Mwizi

Sign up for our Newsletter and
stay informed

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *