Articles

Ukosefu wa ajira unahatarisha Maisha ya vijana na jamii kwa jumla

By Seliphar Muzungu

Twaridhia baghala tukosapo farasi, msemo huu unajionyesha dhahiri katika maisha  ya kijana barobaro, kijana aliyekuwa na ndoto za kufika mbali,kijana aliyewahidi wazazi kwamba pindi atakapo tamatisha masomo yake ya chuo kikuu atayabadilisha maisha yao na wataishi kwa jasho lake na kufurahia matunda ya bidii yao. Kijana aiyekuwa  na ndoto ya kuwa mhandisi tajika katika eneo hili la magharibi na hata nchi nzima. Katika viwango vyake vyote vya masomo alijitahidi sana akikumbuka kwamba ni yeye tu tegemeo la aila yake na ni yeye tu atakaye okoa familia yake kutoka katika lindi la umaskini.

Kutana na John Luseno ambaye ni mkaazi wa kaunti ya Kakamega,eneo bunge la Shinyalu. Luseno anasimulia hadithi ya maisha yake ambayo mwanzo yalikuwa na mwanga wa matumaini lakini mwanga huo ulififia pindi tu alipohitimu kutoka katika chuo kikuu cha Nairobi alipokuwa akisomea uhandisi.

Luseno alianza kwa kusimulia safari yake ya masomo kutokea pale alipofuzu kutoka shule ya upili ya wavulana ya Kakamega ambayo ipo katika viwango vya kitaifa na alama ya A. Matokeo hayo yalimpa Luseno matumaini ya kujiunga na chuo kikuu ambacho amekuwa akikitamani kwa muda mrefu ili kuenda kusomea tasnia ambayo alikuwa akimezea mate miaka yote aliyookuwa shuleni. Wazazi wake walimshukuru Maulana kwa kuwapa mwana mwenye bidii na kuwaondolea shaka ya nini watakachowambia wafadhili na wahisani wa Luseno kama hangefaulu maana kwa miaka yote minne Luseno alikuwa akisoma kwa ufadhili wa kaunti ya Kakamega kitengo cha elimu na wafadhili wengine kama benki ya Equity chini ya mradi wa “Wings to Fly” ambao unaendeshwa na benki hiyo.

Baada ya miezi kadhaa alijiunga na chuo kikuu cha Nairobi ambapo kulingana na masimulizi yake Luseno alipoambiwa kwamba achague kozi ambayo angependa kusomea, hakusita hata sekunde moja alijaza pengo hilo kwa herufi kubwa ya neno uhandisi. Luseno alitia bidii katika masomo yake ya chuo kikuu na matumaini ya kupata kazi atakapofuzu na shahada yake katika uhandisi. Hakujihusisha na mambo ambao vijana wenzake barobaro walikuwa wakijishughulisha nayo chuoni. Maktaba yalikuwa ndio makao yake baada ya kuhudhuria mihadhara, hata ushawishi wa vijana wenzake wa kuenda kucheza densi kwenye vilabu vya Nairobi haukufua dafu,utego huo haukuweza kumnasa.

Baada ya kumaliza masomo yake Luseno alifuzu na daraja la kwanza katika tasnia ya uhandisi. Anavyoeleza Luseno wazazi wake waliandaa sherehe ili kusherehekea kufuzu kwake na kwa matumaini makubwa kwamba baada ya siku chache maisha yao yangebadilika. Luseno angewajengea jumba la kifahari, kuyabadilisha mavazi yao na kubadilisha muonekano wa familia hiyo. Luseno hakujua ni yapi yanamngoja mbeleni, kweli usilolijua ni kama usiku wa giza.

Luseno kama vijana wengine alifunga safari ya kuenda kuanza shughuli ya kutafuta kazi si Nairobi, si Mombasa, si Kisumu na hata Kakamega. Alibisha hodi kwa kila afisi inayojihusisha na maswala ya uhandisi na kuzuru kila kampuni kwa matumaini ya kupata kazi. Ije mvua au jua Luseno hakukata tamaa alijipa matumaini akisema kwamba ipo siku nami nitaweza kuajiriwa.

Jinsi anavyosimulia Luseno mwaka wa kwanza ulikamilika hakuweza kupata ajira afisi alizokuwa akiitembelea swali la kwanza aliloulizwa ni “umetumwa na nani? na unamjua nani afisini humu?” “Maswali haya ambayo niliulizwa kwa kila afisi au kampuni niliyozuru yalinikera sana na kunikata maini. Mimi simjui yeyote wala sina yeyote wa kunituma kwamba nipeleka vyeti vyangu kwa kampuni fulani kitu ambacho ninacho ni stakabadhi zangu na Mungu mimi sina “connections” ufisadi na ukabila bado ni adui mkubwa zaidi hapa nchini. Lakini wana wanaotoka katika familia hohe hahe humu nchini kweli tumepata taabu sana.” Luseno alieleza japo kwa machungu sana

Luseno alieleza kwamba hata baada ya miaka mitatu hakukata tamaa alijaribu tena na tena. Baadhi ya afisi alizozuru aliambiwa kwamba atapigiwa simu baada ya majuma mawili, wengine watamuita pindi tu nafasi ya kazi itakapo patikana na kuambiwa awe mvumilivu.

Baada ya miaka mitano Luseno alikaata tamaa na kuweka vyeti vyake kando maana familia yake ilikuwa ikimtazama yeye tu ili aweze kukimu mahitaji yao. Alipiga moyo konde na kuanza kufanya vibarua vyovyote vile alivyovipata bora tu aweze kupata kidogo cha kutia mdomoni. Aliwalimia watu mashamba, aliwabebea watu mizigo.

Siku moja akiwa katika shughuli zake za kila siku alikutana na rafiki yake wa zamani ambao wanatoka katika eneo hilo la Khayega ambao alisoma nao katika shule ya msingi,  wakiwa wamebeba vifaa vyao vya kazi , huku wamevaliamararu raru. Kwa mara ya kwanza hawakuweza kumtambua Luseno. Walimuita kwa jina kulingana na Luseno vijana wenzake walikuwa wakimuita Johnny kwa kulivuuta jina lake kidogo.  Walishangaa sana kukutana kwa hali ile ambapo kila mmoja ana mengi ya kusimulia. Luseno aliwasimulia hadithi yake na wao pia wakamueleza  kuwa  walihitimu miaka sita iliyopita katika chuo kikuu cha Masinde Muliro kilichoko mjini Kakamega. Edwin na Nabwire wanashahada katika tasnia ya Sayansi ya siasa na utawala wa umma (Political Science and Public Administration).

Wawili hao walimueleza Luseno kazi wanayofanya ambayo ni uchimbaji migodi inayoendelea katika sehemu hiyo. Hii ni kazi ambayo imeshika kasi sana katika eneo bunge ka Shinyalu haswa sana maeneo ya Khayega na viunga vyake.Japo kazi hii inawapa vijana hawa mtaji lakini ni kazi ambayo inamadhara mengi sana.

Luseno alifanya uamuzi wa kujiunga na wenzako japo kuna kundi la vijana  waliowasuta na kuwatania kwamba iweje wao wenye shahada  hawapata kazi na wanajiunga na vijana ambao hata walikatiza masomo yao katika shule ya sekondari na hata wale wa shule za msingi? “Ina maana kwamba shahada zenyu  hazina maana wala manufaa  kabisa? Kwa sabbau mimi ambaye sikufaulu kujiunga na chuo kikuu tuko kimoja? Maana sisi sote tunachimba migodi.” mmoja wa wale vijana aliwambia Luseno na wenzake. Maneno hayo yalimchoma Luseno kama mshale kifuani lakini hakuwa na budi ila kukabiliana na hali yake ya maisha kwa wakati ule maana lisilo na budi hutendwa.

Luseno alianza kazi ya kuchimba migodi na akaizoea na ikawa ndio kazi ambayo anaitegema kukidhi mahitaji yake. Lakini kuna mkasa uliotokea katika shughuli hiyo ya kuchimba migodi ambao ulimpa Luseno wasiwasi na mawazo mengi maana hakujua aendelee na kazi ile ama aikatize maana aliyoyashuhudia yamemtia tumbo joto

Wiki mbili zilizopita baadhi ya vijana wakiume ambao Luseno huchimba nao migodi waliripotiwa kufunikwa na mchanga walipokuwa katika pilkapilka ya kuchimba migodi usiku wa manane ambapo mgodi huo uliporomoka na wenzake hao kufunikwa na mchanga.

Kilichomsikitisha na kumhuzunisha  Luseno ni kwamba mmoja wa wandani wake amefunikwa na mchanga katika mgodi huo. Luseno alipokea habari hizi kwa mshangao na huzuni zaidi. Shughuli ya kuwanusuru wachimba migodi hao ilianza mara moja  ambapo kuna wale waliweza kutoka salama japo na majeraha na kwa bahati mbaya watano kati yao kupoteza maisha yao akiwemo Edwin  rafiki yake Luseno.

Hili ni jambo la kuhuzunisha sana tunapowaona vijana wanafariki kifo cha kutatanisha kama hiki wakiwa katika shughuli ya kujitaftia kipato. Vijana ambao walikuwa na ndoto ya kuwa watu tajika katika jamii lakini kwa sababu ya kukosa ajira, kwa sababu ya kukosa kumjua yeyote kwenye kampuni walifanya uamuzi wa kufanya kazi yoyote ila bora tu wapate chakula na mahitaji mengine ya kimsingi.

Luseno na wenziwe ni baadhi tu ya vijana milioni 73 duniani ambao hawana ajira hii ni kulingana na shirika la ajira la kimataifa “International Labour Organisation” utafiti wa mwaka uliopita 2022. Wanawakilisha asilimia 48.61 ya vijana nchini Kenya ambao wamehitimu lakini wamekosa ajira.

Ni nini maana ya vyeti ambavyo hawa vijana wanamiliki? Vyeti hivi vimegeuka kuwa maridadi tu havina maana wala manufaa yoyote katika maisha ya vijana hawa ambao wamebisha hodi katika kila ofisi, wamezuru kila jumba ambalo wanapata fununu kwamba Kuna nafasi ya kazi, lakini wameambulia patupu juhudi zao zikigonga mwamba na  zimetokomea katika kapu la sahau. Sisemi ni pesa ngapi wamelipa katika hizi afisi ndiposa waweze kupata kazi na zote zikaingia katika mifuko mikubwa isiyojaa ya mameneja, wakuu na wasimamizi wa makampuni na viwanda mbalimbali nchini. Wengine hata wanaulizwa  ni nani wanajua . Nani aliyewatuma jinsi alivyotuelezea Luseno. Kama huna kiunganishi huna lako kama aila yako haijulikani na mkuu yeyote hapa nchini basi wewe na shahada yako  utatembea vyatu vichuchuke, na nguo ziwe mararu  kweli. Ufisadi na Ukabila umechukua nafasi kubwa katika swala nzima la ajira nchini.  Wengi wanasema  lazima ukuwe na “connection” lakini kwa wale hawana “connection” watamlilia nani?

Ni juzi tu, gavana wa kaunti ya Kakamega ameongoza ibaada malum ya vijana watano walifariki katika mgodi wakiwa katika pilka pilka za  kujitaftia mtaji walipoangukiwa na mchanga na kufunikwa. Jambo lilopelekea wao kupoteza maisha na kukatiza ndoto na matumaini yao. Ni jambo la kuhuzumisha Sana maana wao ndio tegemeo la familia zao. Vijana barobaro, vijana ambao walifariki kifo kichungu ambacho wao wenyewe hawakukipangia wala kukifikiria, masomo yao na vyeti vyao vyote vimekuwa bure machoni mwa familia zao.

Wengi wa vijana niliozungumza nao  walisema kwamba licha ya wao kuhitimu na kukosa ajira wamepoteza matumaini  ya kupata  kazi za afisini ni heri kufanya kazi yoyote ile bora tu waweze kukimu maisha yao. Wengi wameingilia jua kali, wengine biashara, wengine kilimo na wengine hata kuingilia biashara za mitandaoni.

Kwa kweli, kila juhudi lafaa kuwekwa ili shida ya ukosefu wa ajira liweze kusuluhishwa.

Related posts
Articles

Brian

Articles

Echoes of Midnight

Articles

Call for Action against Greedy Leadership: Gen Z Calls Them Out

Articles

Call for Peace in Kenya by President

Sign up for our Newsletter and
stay informed

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *