Caroline Boyani
Malumbano na tetesi kati ya viongozi wa kidini, viongozi wa serikali na wanachama wa Vikundi vinavyounga mkono ndoa za jinsia moja yamepiga vyumba vya habari na mitandao. Swala hilo limechochewa zaidi na hatua ya majaji watatu mahakama ya juu kuhalalisha kikundi cha kupigania ushoga (National Gay and Lesbian Human rights commission, NGLHRC) ilhali wakisema ndoa za jinsia moja ni haramu.
Swala hili limechipua hisia mseto wengi wakiwanyoshea vidole majaji hao na kuitaka mahakama iongeze adhabu dhidi ya watakaopatikana wakijihusisha na ulawiti na ushoga. Majaji hao walisema shoga pia ni binadamu na wana haki za kibinadamu.
Katiba ya kenya kipengele cha 162 kinaweka wazi kuwa ulawiti ni hatia na mtu anayepatikana akijihusisha na hayo anaweza fungwa kwa miaka kumi na mitano. Ingawa haiweki wazi adhabu ya wanaojihusisha na ndoa za kike.
Rita , si jina lake kamili, ni mwanadada wa takriban miaka ishirini na tatu. Rita ni mojawapo ya wanaounga mkono hatua ya majaji hao. Analalama kuwa penzi ni penzi kwa hivyo si sawa kumhukumu mtu huku akisema amri kuu Mungu aliyotuachia ni Upendo. “Sheria hizi zilipitishwa na wakoloni na ata baada ya miaka sitini mkoloni anatawala maisha yetu” aliongeza.
Wanaoshiriki kwenye mahusiano ya jinsia moja utengwa na waliokaribu nao. Wengi hawana uhuru wa kujieleza, kupata ajira na wengi wamejeruhiwa na kufukuzwa shule kwa wale ambao wanasoma. Kwa wale wanataka kuunda familia wamenyimwa uhuru wa kuasili mtoto. Hizi zikiwa baadhi ya changamoto wanazopitia. Rita anawaomba Wakenya kukubali uamuzi uliotolewa.
Kwa upande mwingine masheikh katika jiji la Mombasa wana ghadhabu na uamuzi uliotolewa. Wamelaani kitendo hicho wakisema ata kama ni misaada ya nchi za nje wako tayari kutopokea ili kuhakikisha ndoa za jinsia moja zipigwe marufuku.
Sheikh Abu Khamza alilaani kitendo hicho akiuliza kizazi kitaendeleaje ikiwa mwanaume atamwoa mwanaume mwenzake watajifungua vipi. ” Vitabu vya dini vimekataa mahusiano ya jinsia moja, Mungu arati rehemu,” alisema. Alimwomba waziri wa elimu Ezekiel Machogu adhibiti vitabu vinavyouzwa na kuhakikisha haviongelei ushoga. ” Mashirika yamekuja yanayowapotosha wana wetu kwenye mtandao, wachukuliwe hatua” aliomba Abu.
Sheikh Badru Khamis wa Fayaz alitaka majaji hao watatu wachunguzwe. “Tunataka kujua kwa nini walitoa uamuzi huo unaopingwa na dini zote” alinena. “Hatua isipochukuliwa tuko tayari kuenda kwa koti za Afrika Mashariki” aliongeza.
Riziki Juma mwakilishi wa akina mama katika shirika la Supreme Council of Kenya muslims alilalama kuwa akina mama ndio wanaathirika zaidi. Alikashifu vikali huku akionyesha mkeka wa kusalia uliochorwa upinde wa mvua. Aliwaomba wazazi watilie maanani mienendo ya vijana wao na kuwaelekeza kwa njia inayofaa.
Zubeida Njau naye alitaka Rais ajibu ni kwa nini katika maswala yote yanayokumba nchi kama vile uhalifu na baa la njaa hayajashughulikiwa ilhali hayagongi vichwa vya habari kama ripoti za ulawiti na ushoga. ” Wanaosukuma agenda ya kuhalalisha uchafu huu wakome, na kama ni misaada yao hatuitaki wabaki nayo” Njau alielezea kusikitishwa kwake.
Makanisa ya kipentekoste yakiongozwa na Dr Paul Mwaura yaliguzia swala hilo wakisema maji yasizidi unga, watawasilisha mswada bunge hili katiba na sheria ziangaliwe upya.
Maaskofi Elijah Kamau na Alphas Goda waliitaka serikali iwachunguze majaji hao watatu walioenda kinyume cha wakenya. “Mungu atafuraishwa na matendo yetu na tutaangamizwa kama Sodoma na Gomora” alisema Kamau akitaka wote wanaojihusha na mahusiano hayo kutubu.
Je, Kenya itaangamizwa kama nchi ya Sodoma na Gomora wakati wa Lutu au kila mwanadamu ana uhuru wa kuishi anavyoona yastahili? Ni swala la kuwa ndugu mwema ama ni kila mtu aiokoe nafsi yake ila Mungu wetu sote? Hukumu yote twamwachia Maulana.