Articles

Madhara Yatokanayo na Matumizi ya Dawa za Kulevya kwa Vijana

By Seliphar Machoni, Kakamega

Siku zote mzazi hushauriwa  kwamba ukimlea mwana mwema, mui pia mlee. Lakin kwa mama yake Simiyu maji yamemfika shingoni.  Anaonekana akiwa ameketi chini ya mti, huku amejiinamia, akiwa amejishika tama,  akiwaza na kuwazua kuhusu hali na hatima ya mwanawe. Akilini alijiuliza maswali mengi yasiyokuwa na majibu.

“Huyu wangu kageuka  mui nitamlea vipi? Nimefanya kila kitu ili mwanangu aweze kurudia hali yake ya zamani lakini juhudi zangu zote ziliambulia patupu, maskio yake kayatia nta. Ina maana kwamba sitaweza kumrudisha mwanangu katika hali yake ya zamani? Ina maana kwamba nimempoteza mwanangu? Nilikosea wapi mimi katika malezi ndiposa mwanangu akageuka mwehu asiyetambulika,asiye na mbele wala nyuma? Dawa za kulevya  ndicho chakula chake cha kila siku ,nyumbani amepahama sasa yeye ni mwana wa mjini? Masomo nayo akayasusia vitabu sijui alivitupa wapi maskini Simiyu  mwanangu? Haskii la mwadhini wala la mteka maji msikitini. Nitafanya nini ili niweze kumnusuru mwanangu kutokana na jinamizi hili la matumizi ya dawa za kulevya? Mtihani huu mgumu sana kwangu.”

Simiyu  ambaye kwa sasa yeye ndiye gwiji wa kusambaza na kutumia dawa za kulevya mjini Kakamega. Jambo hili lilimhuzunisha na kumtatiza  sana mamake Simiyu.

Simiyu  alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya upili ya Emurumba iliyoko viungani mwa mji wa Kakamega. Simiyu  alikuwa ndiye mwana wa pekee wa Bi Naliaka. Simiyu alikuwa mtoto mtiifu, mpole na mwenye bidii masomoni. Tangu alipokuwa kidato cha kwanza Simiyu  alikuwa akiongoza  kwa kushika nambari ya kwanza. Alikuwa wembe masomoni na kila mwanalimu alifanya lolote lile ili  aweze kuibuka mshindi darasani. Mamake ambaye alikuwa na bidii za mchwa katika biashara yake ya kuuza mahamri, karanga na mchicha sokoni hakukawia kumlipia mwanawe karo.  Alijua fika kuwa mwanawe angesoma kwa bidii na angemfaa badae.

Kidato cha kwanza, cha pili na cha tatu mambo kwa upande wa Simiyu  yalikuwa sawasawa kabisa. Alishikilia nambari ya kwamza masomoni. Alipoingia kidato cha nne hapo ndipo chombo chake Simiyu  kilianza kuenda marama. Simiyu aliabiri meli ya matumizi ya dawa za kulevya na akawa abiria sawasawa hadi pale alipofika katika ng’ambo ya pili. Simiyu alijiunga na kikundi cha wanafunzi waliotumia mihadarati shuleni. Kundi hili lilojiita “kundi la wakuu” liliongozwa na rafiki yake Simiyu kwa jina Wafula. Wafula ni mtoto wa mwanabiashara mashuhuri  na tajika sana mjini Kakamega. Masomo kwa Wafula  hayakuwa na maana alihudhuria vipindi vya masomo siku ambayo yeye mwenyewe ameichagua.

Kwa siku nyingi alikuwa akimshawishi  Simiyu ili kujiunga na kundi  la “Wakuu” lakini Simiyu alikataa kabisa. Siku moja, mtego wa Wafula ulimnasa Simiyu sawasawa. Wafula alimwambia  Simiyu kwamba angependa amsaidie kazi ya ziada aliyopewa na mwalimu wa hisabati siku hiyo nyumbani kwao. Simiyu alikuwa tayari kumsaida rafiki yake maana alijua Wafula ni mbumbumbu katika hisabati.

Alipofika chumbani mwa  Wafula alishangaa sana kuwaona  wanachama wa kundi la “wakuu” chumbani humo, huku wakivuta sigara, wenye pombe mikononi, wengine wakitafuna miraa. Mazingira hayo hayakumfaa Simiyu,lakini Wafula alimshawishi na kumwambia kwamba hawa ni wenzake na kukaa nao hakutamdhuru wala hakutambadilisha. Simiyu aliketi japo shingo upande. Wafula alijiunga na wenzake  na kuanza kutafuna miraa. Mmoja wa wale wanachana alimpa Simiyu sigara. Kwa mara ya kwanza Simiyu  alikata kuipokea lakini kwa ushawishi wa Wafula na “Wakuu” wenzake aliweza kujaribu. Punde tu alipojaribu kwa mara ya kwanza Simiyu alikohoa sana na kuitupa sigara hiyo. Wafula na wenzake walimcheka. Hayakuishia hapo Simiyu alipewa matawi ya miraa ili akatafune. Kwa Simiyu matawi hayo yalikuwa machungu mno na yasiyokuwa na ladha hakujua mbona wanachama hao waliyapenda matawi hayo. Aliyatema mara moja .

“Pole pole  Simiyu utazoea tu, nataka uwe mwanachama asilia wa chama hiki cha “wakuu.”  Masomo bila raha kidogo hayatakusaidia, furahiya maisha wewe ni kijana barobaro masomo hayaishi yalikuwepo wakati wa mababu zetu hadi sasa na hata sisi tutayaacha. Kwa sasa kunywa hii utakuwa sawa kabisa.”  Wafula aliyasema haya akimkabidhi Simiyu glasi iliyojaa Pombe.

Kwa muda  Simiyu alitazama glasi hiyo asijue la kufanya. Akilini  alikuwa anajiuliza maswali si haba, vipi mama yake akijua kwamba alimfuata Wafula hadi nyumbani kwao baada ya yeye mwenyewe kumkanya  na kumsihi aepukane na Wafula? Atajinasua vipi  kutoka katika mtego huo wa wanachama hawa wasiomtakia mema?

Juma aliukumbuka wosia wa mamake  kuhusu matumizi ya dawa za kulevya, alikumbuka ndugu yake mama yake aliyeaga dunia kutokana na saratani ya mapafu iliyosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya. Alimkumbuka Nekesa binti ya jirani yake kule nyumbani ambaye kwa sasa amegeuka mwehu kwa sababu ya matumizi ya dawa za kulevya kipitiliza. Aliwangalia wanachama wale ambao kwa wakati ule walikuwa wakimtazama kwa macho ya kumshawishi . “Kunywa hata funda moja Simiyu hutalewa wala haitakudhuru.”  Wafula aliskika akimwambia Simiyu.

Simiyu alipiga moyo konde na kusema liwalo na liwe ni mara moja tu.  Aliyafunga macho na kumimina pombe yote mdomoni  na kuiweka glasi kwenye meza. Wanachana hao walimshangilia na kumsifu. Huku Wafula akimkaribisha rasmi katika kikundi cha “wakuu”. “Wewe sasa ni mwanachama rasmi wa kikundi hiki cha “wakuu” karibu sana na kando na starahe hii tutakufunza jinsi ya kupata pesa kwa kuuza miraa utapata pesa nyingi sana.”  Wafula alimueleza  Simiyu ambaye kwa wakati huo alikuwa hajielewi  ameanza kuona mbili mbili.

Siku zilivyosonga ndipo Simiyu alivyojiingiza zaidi katika matumizi ya dawa za kulevya. Mara nyingi alikosa kuhudhuria vipindi darasani na hata kukosa kufika shule. Walimu walishangazwa sana na tabia yake  Simiyu ambayo hawakuielewa kabisa. Siku moja mwalimu wa historia  alimuita Simiyu  na kumhoji  maana alikuwa amefeli sana katika jaribio la historia alilolifanya. Simiyu hakuwa na jibu lolote alibaki amemtazana mwalimu tu.

Mama yake Simiyu  alipoitwa shuleni ili wamueeleze tabia za mwanawe, siku hiyo  Simiyu hakuwa shuleni  hata baada ya kumuaga mamake na kumwambia kwamba anaenda shuleni hakufika shuleni.  Mwakilishi wa kidato cha nne alipoulizwa alidokeza  kwamba alimuona  Simiyu na wanachana wa kikundi cha “wakuu”  mjini Kakamega . Mama mtu alibaki ameduwaa nakushangazwa na tabia hiyo ya mwanawe.  Hakujua kwamba hiyo ndiyo ilikuwa siku yake Simiyu  ya mwisho shuleni .

Kwa sababu ya uraibu huo,  Simiyu hakurudi shuleni tena.  Simiyu kwa sasa utamuona akipita pita mitaani mjini Kakamega huku akitafuna miraa, mfukono ana chupa ya pombe , nywele zake tim tim na nguo zake mararu raru. Akitembea ungedhani ataanguka wakati wowote. Meno pamoja na mdomo wake umepoteza rangi yake asilia. Simiyu angeonekana akizungumza na watu wasioonekana hata kuwakimbiza .

Juhudi za mama yake kuweza kumnusuru kutokana na  matumizi ya dawa za kulenya azikufua dafu kwani Simiyu alikuwa amezama na kuzama zaidi. Mama mtu alikata tamaa na kusema liwalo na liwe aliyavulia nguo acha akayaoge.

Simiyu ni mfano tu wa baadhi  ya vijana wanaotumia dawa za kuevya eneo hili la magharibi mwa nchi. Kulingana na utafiti uliofanywa mwaka jana kati ya mwezi wa Septemba hadi Desemba na shirika la kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya nchini (NACADA) unaonyesha kwamba  eneo la maghabiri mwa Kenya linaendelea kurekodi visa vingi vya matumizi ya dawa za kulevya ukilinganisha na eneo la pwani ambapo hapo awali lilikuwa likishkilia nambari moja katika matumizi ya mihadarati.

Utafiti huo wa Nacada ulionyesha  kwamba asilimia 23.8 ya idadi ya watu eneo la magharibi wamebugia sana utumizi ya  dawa za kulevya na vileo haswa sana pombe haramu.

Katika eneo la pwani matumizi haya yako katika asilimia 13.9 ya idadi ya watu wanaotumia.  Eneo la kati mwa nchi likishikilia nambari ya tatu na asilimia 11.4 ya idadi ya watu wanaotumia dawa za kulevya na pombe.

Kwa undani ripoti hiyo inaonyesha kwamba eneo la magharibi linaongoza kwa matumizi mabaya ya dawa za kulevya na pombe haramu nchini Kenya.

Katika mwaka wa 2017, matumizi ya  madawa ya kulevya na pombe katika eneo la magharibu yalikuwa asilimia 13.4 lakini asilimia hii imekuwa ikipanda kila uchao kufuatia ongezeko la matumzi haya.  Mwaka jana  watu asilia 11.4 walikuwa watumizi wa pombe haramu ‘chang’a’ kutoka asilimia 6.   

Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Bwana Victor Okioma alisema kwamba kama shirika wataweka mikakati inayofaa ili kupunguza matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana  eneo la magharibi.

Wito umetolewa kwa vijana kuepukana na makundi ambayo yanaweza kuwashawishi kutumia dawa za kulevya na siku zote kutafuta habari kuhusu mihadarati na madhara yake kabla ya kutumia.

Serikali ya kaunti ya Kakamega na kaunti jirani  imeombwa kuelimisha vijana kuhusu madhara ya dawa ya kulevya na kujenga vituo vingi vya marekebisho kwa wale ambao tayari wameathirika kama vile Simiyu na wenzake. Pia kutoidhinisha ugemaji wa pombe haramu bila idhini kutoka  kwa shirika la Kenya Bureau of Standards (Kebs) ili kuwaokoa vijana kutokana na matumizi ya  dawa za kulevya nchini.

Related posts
Articles

Nairobi's Transformation: From Green City to Concrete Jungle

Articles

Kenya's Ongoing Battle with Malaria: Progress, Challenges, and Strategies

Articles

Mama Lucy Kibaki Eye Hospital Continues to Restore Vision

Articles

Empowering Obunga Fish Traders

Sign up for our Newsletter and
stay informed

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *