Articles

Machungu ya wafanyikazi wa Nyumbani

Caroline Boyani Oyaro

Riziki, ambalo si jina lake sahihi ana miaka arobaini na mitano na ni mama ya watoto wanne. Anaonekana kuzama katika fikira huku kasononeka usoni. Yeye ni mkaazi wa Majengo, kaunti ya Mombasa. Riziki amekuwa akifanya kazi ya uyaya kwa mwongo mmoja sasa. Ingawa anajaribu kutabasamu ili kuficha huzuni wake, machozi yanapata nafasi na kumdondoka. Katika miaka aliyofanya kazi hii, amewatumikia waajiri waliomdhamini na kumchukulia kama mmoja wao, na kunao waliomtia machungu asiweze kuyasahau.

Kwa miezi minane amekuwa akimfanyia mwajiri wake kazi katika hosteli za wasichana huku Mombasa na hajalipwa hata shilingi moja. Mwajiri wake pia hajakuwa akishughulikia maslahi kama vile chakula. Ni haki ya kila binadamu kuwa na lishe, mavazi ya kujisitiri na chumba kinachofaa cha kulala kulingana na katiba ya Kenya na kanuni za maslahi za haki za kibinadamu . Imebidi Riziki abuni mbinu za kujikimu akitumai siku njema itafika. Anatumia kilio chake cha haki kitapata maskio na kuwanusuru wengine kama yeye. Jukumu la Riziki ni kusafisha hosteli na kuwaandalia chakula wanafunzi hao.

Ingawa mwajiri amemnunulia mtungi wa gesi na jiko la kupikia, pesa anazompa kwa ajili ya kununua chakula hazitoshi na hata baada ya kuwauzia wanafunzi hao chakula hapaswi kuchukua ata shilingi kwa matumizi hayo. Na ikiwa wanafunzi watasita kununua chakula humo, Riziki hatakua na cha kukula kwani kula kwake kunategemea wanafunzi watakao kula kwa hosteli. Kuna muda mwajiri wake alimsingizia kujiwekea sehemu ya kipato alichopata kutokana na kuuza chakula hicho. Kila anapoomba mshahara wake mwajiri hulaumu hali ngumu ya maisha ila subira yake inafifia. Hali hii imepelekea Riziki kutafuta vibarua vinginevyo kama vile kuosha nguo.

Baadhi ya wanafunzi anaowalinda katika hosteli waliharibu pasi waya ya WI-Fi na tajiri kutishia kupunguza pesa izo kutoka kwa mshahara wake. Haya ni kati ya masaibu yanayowakumba wafanyikazi wa nyumbani. Wengi wao hawajui haki zao na hawana wa kuwanusuru ila Mungu. Riziki ni miongoni mwa wafanyikazi wenye masomo ya chini, wachochole na wanyonge, wengi wao wakiwa watoto na akina mama. Katiba ya Kenya katika kipengele cha 53 na Children’s Act, 2022 inapiga marufuku ajira ya watoto walio chini ya miaka kumi na minane.

Wafanyikazi wanachukuliwa kama viumbe wa kuonekana na si kusikizwa. Kenya ina wafanyikazi asilimia milioni mbili kulingana na ripoti ya sensa (KNBS, 2020). Mfanyikazi anafaa kufanya kazi masaa hamsini na mawili kwa wiki huku akipumzika masaa kumi na mawili kila siku. Zaidi ya masaa hayo mwajiri wake anafaa kumlipa marupurupu kulingana na ilani ya sita ya kudhibiti mishahara . Kando na haki za kibinadamu , katiba ya Kenya na mashirika ya wafanyakazi ilizindua haki zaidi za wafanyikazi. Mfanyikazi wa nyumbani anastahili siku mbili za kupumzika kila wiki. Yuko na haki ya siku thelathini ambao ni mwezi mmoja wa likizo ya mwaka akipokea mshahara wa mwezi huo. Anapokuwa mgonjwa anafaa kupewa likizo ya ugonjwa, likizo ya uzazi na kushughulikiwa kiafya. Kando na katika kuna vipengele vingine kama Health Act 2007, Labor Relations Act 2007, Sexual offences Act 2006 na Employment Act 2007 zinazomlinda mfanyikazi wa nyumbani.

Kumekuwa na visa vya waajiri kuwalaghai na kuwanyanyasa wafanyikazi. Wengi wakisalia na makovu ya majeraha, kukemewa na kunyimwa mishahara. Wafanyikazi wengi hawaripoti visa hivi kwa woga ila walio na ujasiri huripoti. Baadhi ya visa vinavyoripotiwa huambulia patupu kwani waajiri wana pesa za kutoa ‘kitu kidogo’ ili kuwafumba macho askari. Waajiri wengine ata hudai wafanyikazi hao ni jamaa yao. Baada ya kutafuta usaidizi mwajiri wa riziki amekubali robo tatu za mishahara wake na ahadi ya kulipa salio la robo kabla ya mwaka kutimilika.

Wafanyikazi wa nyumbani ni miongoni mwa sekta ya ndani inayochangia pakubwa katika maendeleo ya nchi. Mashirika ya kupigania haki ya binadamu yamebaini mikakati ya kuwaelimisha watu dhidi ya kuwaajiri watoto na kuwadhulumu wafanyikazi. Ni wajibu wa kila mtu ikiwemo serikali kuhakikisha mahusiano baina ya wafanyikazi na waajiri yameboreshwa. Miaka sitini baada ya uhuru tumepiga hatua ila mengi yanasalia kutiliwa mkazo. Tulimng’oa mkoloni mbeberu ila mizizi yake ilichanua na kukita ndani yetu Waafrica. Ni kinaya Mwafrika mwenzako kukutesa zaidi ya yule waliyemfukuza. Hata baada ya miaka sitini baada ya uhuru, wafanyikazi hawajihisi huru.

Related posts
Articles

Digital Activism and the Youth Bravado (Millennials and Gen Z)

Articles

SHOULD WE ADOPT STRATEGIC AMBIGUITY AS FOREIGN POLICY?

Articles

KENYA’S FINANCE BILL 2024, IN A NUTSHELL

Articles

Mwizi! Mwizi! Mwizi

Sign up for our Newsletter and
stay informed

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *