Imeandikwa na Ahmed Karama
Usalama ni nguzo muhimu katika maisha ya kila binadamu, jamii na taifa kwa jumla. Bila usalama, maendeleo na ustawi wa watu hupungua sana. Jamii yenye usalama huwa na mazingira bora ya uwekezaji, biashara, elimu, na huduma nyingine za kijamii. Mfumo thabiti wa usalama huzuia machafuko, vurugu, na vita vinavyoweza kurudisha nyuma maendeleo ya taifa. Usalama hulinda haki za binadamu, utambulisho wa kijamii na maadili dhidi ya uharibifu au vitisho, hata hivyo kisiwa cha amu kimeendelea kukumbwa na changamoto za kiusalama ambazo mara nyingi zimeathiri maisha ya wakaazi na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kisiwa cha amu ni moja ya visiwa vikubwa katika kaunti ya lamu. Kisiwa hichi kimebeba idadi kubwa ya watu ambao wanaendelea kuongezeka kila kukicha. Kulingana na takwimu kisiwa cha amu kina takriban watu elfu ishirini na watano waliotawanyika katika vijiji mbalimbali kama vile mji wa kale wa lamu, shela, matondoni na kipungani. Licha ya hii idadi kubwa ya watu na ukubwa wa kisiwa hichi, inashangaza kuona kuwa kituo cha polisi ni kimoja pekee kinachopatikana katika mji wa kale wa lamu. Je watu wa shela, matondoni na kipungani hawana haki ya kulindwa?
Uhaba huu wa vituo vya polisi na upungufu wa maafisa wa usalama umechangia pakubwa kuzorota kwa usalama hasa katika maeneo ya matondoni na kipungani. Wengi wakililia na kupendekeza kuwepo kwa kituo cha polisi katika eneo la matondoni ambako visa vya utovu wa usalama vimeongezeka katika siku za hivi karibuni.
Kijiji cha matondoni kipo takriban kilomita nane kutoka mji wa lamu kwa barabara ya ndani ya kisiwa ambapo ndipo kinachopatikana kituo cha polisi. Kwa mashua kupitia bahari, safari ni karibu dakika 30 kutegemea upepo na aina ya chombo.
Kijiji cha kipungani kiko umbali wa takriban kilomita kumi na tano kupitia barabara ya ndani ya kisiwa. Safari ya gari au bodaboda huchukua dakika 35–45 kulingana na hali ya barabara. Kwa njia ya bahari safari inachukua takriban dakika 20–30 kutegemea upepo na aina ya chombo.
Tuangalie umbali wa vijiji hivi viwili kutoka palipo kituo cha polisi alafu tujiulize je maafisa wa polisi hufika maeneo kama haya kushika doria na kuimarisha usalama ama wakazi wa maeneo haya neno usalama wanaliona tu kwenye kamusi?
Usalama ni haki ya kila mkenya na ni msingi wa maisha bora, maendeleo endelevu na amani ya kudumu. Wakazi wa matondoni na kipungani wana haki ya kulindwa kama wakenya wengine.