WritAfrica

DHULUMA ZA HUDUMA

Imeandikwa na Ahmed Karama 

Ili taifa lipige hatua lazima wananchi wake walipe ushuru ambao unatumika katika kuendeleza shughuli za kitaifa. Moja ya jukumu la uongozi wa taifa ni kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma wanazohitaji tena kwa urahisi. Ni matarajio ya walipa ushuru kuwa wanapotaka usaidizi wa kiserikali waupate bila vikwazo. Inapotokea kuwa mwananchi analipa ushuru ila hapati huduma basi hali inakuwa si shwari .

Watu kutoka kaunti ya lamu ni wakenya kama wakenya wengine na wao pia wanalipa ushuru kama wazalendo wengine wanavyolipa ila ikifika kwa kupokea huduma hali inakuwa si hali. Inasikitisha kuona mkenya anaenda katika ofisi ya serikali kutaka huduma ila anakaribishwa na kufuli kubwa sana. 

Moja ya ofisi ambayo ni muhimu sana lamu hasa katika kisiwa cha amu ni ofisi ya leba maana ukiukaji wa haki za wafanyikazi umekithiri sana. Wafanyikazi wananyanyaswa na kudhulumiwa na waajiri wao ila hawana pa kukimbilia maana ofisi pekee yenye kuwasaidia imefungwa, watu kama hawa wakimbilie wapi?

Ni takriban miezi mitatu sasa katika kisiwa cha amu hakuna afisaa wa Leba. Tangu afisaa aliyekuwepo kupewa uhamisho na kupelekwa kilifi, ofisi ya leba amu imebaki mahema tu. Ukifika ofisini unalakiwa na karani ambaye hajui akusaidie vipi, cha msingi labda kukupa matumaini kuwa huenda hivi karibuni afisaa akapatikana na msaada kutoka. Kibaya  zaidi ni kuwa mara nyingi hata huyo karani huingia mitini unapofika ofisini unakaribishwa na kufuli kubwa sana inayokukodolea macho na mavumbi yanayokufuza kwa kuchemua.

Baada ya kuhangaika kufanya kazi na kulipa ushuru wa taifa, kitu kikubwa mwananchi anachotarajia kutoka kwa serikali ni huduma na utetezi ili haki zake zisikiukwe. Ikiwa muajiriwa atakandamizwa na muajiri wake na serikali nayo imkandamize kwa kutompa huduma na utetezi anaohitaji huyu mtu atakimbilia wapi? Serikali inapaswa kuwa ngao na mlinzi wa wananchi wake kwa maslahi na faida ya pande zote mbili. 

Ni jukumu la serikali kuhakikisha wanachi wake wanakuwa na mazingira bora ya kufanya kazi ili mwisho wa siku waweze kumudu kulipa ushuru na taifa lipige hatua kwani taifa ni watu.

Tags:

No tags assigned to this post.

Related Posts

Top Categories

Trending News

You Know We are Kin, I and You
The People’s Peace
Siasa Ya ID
UFISADI TIA  ZII
HEALTH SERVICE CHRONICLES
Protest is Not A Crime - Article 37

Subscribe to Our Newsletter

Join our vibrant community of young poets, writers, and illustrators.