By Tabitha Marion
Elimu bora imekuwa tangu jadi ahadi za kila anayegombea uongozi wa kisiasa nchini Kenya.
Tulianzia na kuondoa ujinga kupitia elimu. Tukapata ahadi za elimu ya bure katika shule. Na
kwa sasa, tumefikia kiwango cha kuiboresha elimu kwa kubadili mfumo wa elimu. Hatua hizi
zimekuwa bora mno tukizingatia lengo kuu la uanzilishi wa elimu. Ilhali, swala la kutia fikra ni
kama kwa kweli elimu imepata kuboreshwa. Kwa kiwango gani imeboreshwa na kama
wanafunzi wanafaidika na mabidiliko haya na uboreshaji huu.
Katika kitongoji cha Soysambu kuliko shule ya msingi ya Fanaka, tutapata taswira ya hali ya
elimu. Wanafunzi kama kawaida wako mbioni na baridi ya mapambazuko wanaharakisha kufika
shuleni. Wengi wao wamevalia sare zilizoraruka na bila viatu miguuni. Lango kuu la shule
linakaribia kuanguka lakini limejizatiti kulibeba jina la shule fanaka ambalo halisomeki kutokana
na rangi kujifuta.
Naingia shuleni pamoja na wanafunzi na mandhari yanabadilika. Kuna uvundo mkali unaotawala
hewa ya shule. Kutazama huku na kule, macho yakaanguka kwenye maji taka yaliyokusanyika
na kufwata mkondo mmoja kuelekea palipo na shimo ya taka kando ya lango kuu. Maji meusi
yaliyojaa vinyesi na mkojo pamoja na taka za jikoni.
Nikashika mwendo kuelekea madarasani. Madarasa yenyewe ni mbovu mithili ya vibanda vya
sokoni. Wanafunzi katika darasa moja walikuwa wengi kiasi cha kufinyana wanafunzi wanne
kwenye dawati moja. Sakafu la darasa hilo lilikuwa na mashimo kila sehemu. Ubao wao ulikuwa
umevunjika na hata kutishia kuanguka. Ni saa tatu asubuhi na hamna dalili ya masomo
kuendelea katika shule la Fanaka. Ghafla mwalimu aliyeonekana kutambulika kama mwalimu
mkuu akaingia darasa hilo.
"Hujambo wanafunzi?"
Kwa pamoja wanafunzi wakajibu kwa sauti zilizojaa hofu, "Hatujambo mwalimu mkuu."
"Nami ni barua za wanafunzi ambao wako na deni ya karo. Ukilisikia jina lako kujia barua na
ubebe mkoba wako urudi nyumbani hadi mzazi atakapokamilisha malipo. Juma, Mary, Rita…"
Majina yaliendelea kusomwa na wanafunzi kuondoka mmoja baada ya mwengine hadi barua
zilipoisha. Darasani kukasalia wanafunzi tano tu na mwalimu mkuu akaondoka.
Kwa muda huo hadi kengele ilipokirizwa kuashiria mapumziko hadi mchana hakuna mwalimu
aliyeingia darasani. Shuleni Fanaka wanafunzi waliosalia kwa sababu za kumaliza karo
walicheza bila ya kusoma chochote. Wakati wa kula chakula cha mchana, wanafunzi walipiga
foleni nje ya jikoni. Waliokuwa wanapakua chakula walikuwa wanatiririkwa na jasho na
kudondoka kwenye sufuria iliyobeba chakula cha wanafunzi. Wapishi wengine mara walipiga
chafya bila ya kufunika midomo. Wakaanza kupakua chakula. Kila mwanafunzi alichotewa wali
na maharage kiwango kidogo baada ya kupeana pesa kwa mpishi aliyesimama kando ya foleni
kudai pesa na sura iliyokunjana. Wanafunzi wasio na pesa walisalia darasani na kupiga hadithi
zisizo na mwisho kupitisha masaa.
Nikaamua kutembea shuleni kuona hali ya shule kwa ujumla. Nilighadhabishwa nilipoona hali
ya vyoo katika shule. Mnuko mchafu wa vinyesi na mkojo ilisheheni hewa mahali pale. Vyoo
vilijaa uchafu na kutapika taka nje ya milango. Uchafu huo ulitapakaa na kuharibu mazingira
hayo.
Nilipochoshwa na hali hiyo nikaelekea maktabani nitulize akili na vitabu. Kuingia ndani
nalitazamwa na meza iliyojaa vitabu vilivyochanika na kuraruka. Kutazama huku na kule,
sikupaona pahali pa kuketi wala vitabu vingine vilivyowekwa vizuri. Kumjongea niliyemdhania
kuwa mkuu wa maktaba nikamuuliza, "Hujambo? Naweza pata vitabu vya hadithi?"
Akanitazama na kunieleza,"Samahani mwalimu vitabu haviko kwa sasa. Wanafunzi hawajalipa
karo sasa hatuna pesa za kununua vitabu bado."
Nilisikitishwa na maneno hayo na kuondoka maktabani. Nikaelekea kujikinga katika darasa
lingine mvua ilipoanza kunyesha. Nikawapata wanafunzi wakisukuma madawati kwa kona moja
ya darasa. Wakachukua ndoo na kuanza kutega maji yaliyotona darasani kupitia paa la darasa.
Mvua sasa ulinyesha nje na ndani kwa sababu ndoo hizo zilijaa na maji yakaanza kumwagika
darasani. Punde tu mvua uliposita kunyesha, wanafunzi wakazamia kuchota na kumwaga maji
yaliyojaa darasani.
Kengele ilipogongwa ya kuashiria masaa ya kurudi darasani kwa masomo ya jioni, niliwaona
walimu wakiondoka afisini na kuelekea madarasani. Walimu walipofika darasani waliandika
maswali ubaoni kama kazi ya nyumbani kwa wanafunzi. Baadaye wanafunzi na mikoba yao
wakaondoka shuleni kuelekea nyumbani. Masomo ya siku katika shule ya Fanaka kutamatika.
Msemo ni bora elimu kwa sasa badala ya elimu bora. Hili ni taswira kama ilivyo katika shule
nyingi kwa sasa. Walimu wanapolalama hawajalipwa wanakosa hamu ya kufunza. Walimu
wakuu katika shule wanatoza wazazi karo ghali kusimamia ujenzi na uendelezaji wa shule
sababu kuu ni serikali haijajukumika kutuma pesa katika shule. Wazazi wanaishi wakidaiwa
mara karo, mara vitabu, mara kalamu au hata mayai na nyama ya 'project' inavyosemekana.
Wanafunzi wanapitia hali ngumu kutumwa nyumbani mara kwa mara kuleta karo. Shuleni
mazingara nayo sio ya kutunza afya zao. Madarasa yalitoboka mashimo kutishia hata usalama
wa watoto shuleni. Isitoshe, ni shule ndio, ilhali elimu wataipata wapi?
Elimu inapofanyika kuwa ghali kwa kiwango hiki, mtoto wa maskini ana lake kweli? Hali ya
masomo shuleni inafaa kuzingatiwa kwa undani.