WritAfrica

Je, ambulensi ya Lamu ni tuktuk au mkokoteni?

Yusuff Baishe 

Shirika la Siasa Place liliandaa baraza katika mradi wao wa WritAfrica pale Lamu Fort, ambapo wakazi wengi wa Amu walihudhuria. Wakati wa mkutano huo, Bwana Edward alizua mjadala kuhusu jambo ambalo halikumfurahisha katika Hospitali ya King Fahad Referral. Alisema kuna tuktuk ambayo ni inapaswa kufanya kazi kama ambulensi hapa Kisiwa cha Amu, lakini haisaidii wagonjwa kama inavyopaswa.

Bwana Edward alisema, “Inaonekana kama ni kwa ajili ya kuonyeshwa tu(show), na haiwasaidii sana wamama wajawazito, hasa wakati wa usiku. Lakini utaona wagonjwa wanaletwa hospitali kwa mikokoteni. Kwa nini hiyo tuktuk isilale mjini ili kuchukua wagonjwa, badala ya kulala hapa hospitalini?”

UCHUNGUZI WA KINA 

Kufuatia malalamiko hayo yaliyoibuliwa na wakazi wakati wa mkutano huo, nilitembelea Hospitali ya King Fahad Referral ili kupata ufafanuzi zaidi.

Mmoja wa wahudumu wa pale alisema kuwa tuktuk hiyo ililetwa na Ahmed Medo, ambaye ni MCA wa kuteuliwa wa Mkomani na pia mgombea anayepania kiti cha Ubunge mwaka 2027. Alieleza, “Siku ile private wing ilipofunguliwa huku juu, King Fahad ilipokea msaada wa vitanda na hiyo tuktuk kama ambulensi. Ninavyojua, tuktuk hiyo inafanya kazi pale hospitalini; ikiwa kuna mgonjwa anayehitaji kufuatwa, huenda kumleta.”

Ili kupata ukweli zaidi, niliamua kuzungumza na baadhi ya wakazi wakiwa hapo hospitali.

Mwanahalima Abuu, mama wa watoto wawili na mkazi wa Kisiwa cha Amu, alisema, “Mimi binafsi huwa naiona tu hapa hospitalini. Sijawahi kuona ikibeba wagonjwa. Wakati mwingine ninaweza kupishana nayo barabarani, lakini sijui kama inafanya kazi au la.”

Salma Mahamud, ambaye alikuwa akisubiri huduma hospitalini hapo, aliongeza kwa masikitiko, “Mimi nimeshuhudia mgonjwa mzee akiletwa hospitalini kwa mkokoteni. Sikuwa peke yangu, nilikuwa na marafiki zangu. Wallahi, ni jambo la kusikitisha kuona hivi wakati tuktuk iko hapa hapa hospitalini.”

MTAZAMO WA HOSPITALINI 

Hata hivyo, nilipouliza mhudumu mwingine wa hospitali, alitoa mtazamo tofauti. Alieleza kuwa miundombinu ya Amu ni changamoto: “Barabara na vichochoro vya Kisiwa cha Amu ni vigumu kupitika; kuna maeneo ambayo tuktuk haiwezi kufika. Kuhusu mkokoteni, mimi sijaona; labda ilikuwa zamani. Kingine ni kuwa jamii yetu ya Amu wanapenda sana kutumia boda-boda kuleta wagonjwa wao hospitalini, hata kama ni wazee.”

Tags:

No tags assigned to this post.

Related Posts

Top Categories

Trending News

UNSAFE AND NEGLECTED SCHOOL TOILET S
THE GIG WORK TRAP
JUGGLING CARE AND CLICKS
EXPENSE DILEMMA
ENVIRONMENTAL POLLUTION ON NATURE
ABACHA MOVIN-BURDEN ON ORDINARY COMMUTERS

Subscribe to Our Newsletter

Join our vibrant community of young poets, writers, and illustrators.