WritAfrica

PLASTIKI ZA KIFO

IMEANDIKWA NA AHMED KARAMA 

Katika siku za hivi karibuni, wakazi wa Kisiwa cha Amu wameingiwa na hofu kufuatia ongezeko la vifo vya punda wanaoaminika kufariki kutokana na kula taka za plastiki. Tukio hili limezua mjadala mkali kuhusu hali ya usafi wa mazingira kisiwani humo na athari za taka za plastiki kwa wanyama na mazingira kwa jumla.

Punda ni miongoni mwa wanyama muhimu sana kwa wakazi wa Amu. Wengi wao hutegemea punda kwa shughuli za kila siku kama vile kubeba mizigo, bidhaa za dukani na hata vifaa vya ujenzi kutokana na changamoto ya barabara nyembamba na zisizopitika kwa magari katika mji wa kale wa Amu. Hivyo basi, kifo cha punda si hasara kwa mmiliki pekee bali pia ni pigo kwa uchumi wa familia na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi, punda wamekuwa wakila plastiki wakiwa wanazurura ovyo katika mitaa ya Amu wakitafuta chakula. Kutokana na ukosefu wa mifumo bora ya ukusanyaji na utupaji taka, mifuko na vipande vya plastiki husambaa mitaani, na punda wasio na uangalizi huvitafuna wakidhani ni chakula. Plastiki hizo hushindikana kumeng’enywa tumboni, na hatimaye husababisha kuziba kwa njia ya chakula, maumivu makali, na kifo.

Zaidi ya hilo, wakazi wa Amu wamelalamikia ukosefu wa maeneo rasmi ya kutupa taka. Wengi wao hulazimika kutupa taka mitaani au kandokando ya barabara kutokana na ukosefu wa magari ya kukusanya taka mara kwa mara. Hali hii imepelekea ongezeko la taka zisizo na udhibiti, na hatari kwa wanyama kama punda wanaozurura mitaani.

Serikali ya kaunti ya Lamu wana jukumu la kuongeza juhudi katika utekelezaji wa marufuku ya plastiki, ambayo ilipitishwa kitaifa mwaka 2017 lakini utekelezaji wake umekuwa hafifu katika maeneo ya visiwani. Bila hatua madhubuti, huenda vifo vya punda vikaendelea, na hali ya usafi wa mazingira Amu kuzorota zaidi.

 Ongezeko la vifo vya punda kutokana na kula plastiki kisiwani Amu ni ishara ya changamoto pana ya uchafuzi wa mazingira. Ni wajibu wa kila mwananchi, pamoja na serikali kuhakikisha taka zinadhibitiwa ipasavyo. Kwa kufanya hivyo, hatutawalinda  wanyama wetu pekee zbali pia tutahifadhi uzuri na urithi wa mazingira ya kipekee wa Kisiwa cha Amu.

Kila punda anayekufa kutokana na plastiki ni onyo kwamba mazingira yetu yamechafuliwa kupita kiasi. Tunahitaji elimu ya mazingira na sheria kali za kudhibiti taka. 

Tags:

No tags assigned to this post.

Related Posts

Top Categories

Trending News

COMMUNITY EFFORTS VS CRIME
WHERE WATER PASSES
COMMUNITY GROWTH THROUGH SOCIAL HALLS
PASSPORTS IN A FLASH
The Habit of our leaders
Stop GBV

Subscribe to Our Newsletter

Join our vibrant community of young poets, writers, and illustrators.