Imeandikwa na Ahmed Karama
Kazi bila malipo ni sawa na jembe lisilo na mkulima. Msemo huu umebeba maana halisi ya hali ya wahudumu wa afya kaunti ya lamu. Kwa muda wamekuwa wakilalamikia kucheleweshwa kwa mishahara yao ila malalamishi yao yamekuwa yakiingilia sikio la kulia yakitokea sikio la kushoto. Serikali ya kaunti ya lamu wamegeuka kuwa sikio la kufa ambalo halisikii dawa. Wamekuwa hawasikii la mwadhini wala mteka maji msikitini.
Unawezaje kufanya kazi bila malipo? Ama wacha nibadilishe swali, unawezaje kufanya kazi alafu usile? Usipokula leo kazi kesho utafanya vipi? Na kama ni lazima ule ndio upate nguvu za kufanya kazi, hiki chakula utanunua na nini kama hulipwi? Haya si maswali yangu bali ni maswali ambayo wahudumu wa afya kaunti ya lamu wamekuwa wakiyauliza kwa muajiri wao, serikali ya kaunti ya lamu.
Wahudumu wa afya kaunti ya lamu wamekuwa wakicheleweshewa mishahara yao jambo ambalo linazorotesha utoaji wao wa huduma kwa wagonjwa wanaotembelea hospitali na vituo vya afya.
Kwa muda sasa wahudumu wa afya hawajaongezewa mishahara na wametaka kutekelezwa kwa nyongeza ya mshahara ya asilimia sita iliyoidhinishwa na tume ya mishahara na marupurupu (SRC) pamoja na malimbikizo yake.
Miongoni mwa madai yao ni kupandishwa vyeo mara moja kulingana na makundi ya kazi wanayostahili, pamoja na kuundwa kwa makubaliano ya pamoja ya kazi (CBA) kwa kada zote, kamati ya mazungumzo na ufuatiliaji wa utekelezaji wake. Aidha, wanataka walipwe marupurupu ya mikataba iliyomalizika na wafanyakazi wa mikataba kuingizwa kwenye ajira ya kudumu.
Wahudumu hao pia wameitaka serikali kuhakikisha mishahara inalipwa kwa wakati kila mwezi, sambamba na kutekelezwa kwa nyongeza ya mishahara ya asilimia 6 iliyoidhinishwa na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kwa mwaka wa kifedha 2024/2025. Wanasema ucheleweshaji wa malipo umeathiri maisha yao binafsi na motisha kazini, huku wagonjwa pia wakikosa huduma bora kutokana na hali hiyo. Kama methali isemavyo: “Haki ya mfanyakazi ni ujira wake.”
Kwa jumla, madai haya yameelezwa kama ya msingi kwa mustakabali wa sekta ya afya Lamu, kwani yanahusiana moja kwa moja na ustawi wa wahudumu na wagonjwa. Wadau wanatoa wito kwa serikali ya kaunti kushughulikia madai haya bila kusita ili kuepusha migomo zaidi na kulinda maisha ya wananchi wanaotegemea hospitali na vituo vya afya vya umma.
Afya bora ni mtaji wa maisha