Imeandikwa na Alex Maina
Wakaazi wa Kapchumba, Kambi Thomas, Keroka, na Roadblock katika Wadi ya Kiplombe wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kupata huduma za afya. Kwa kukosa kituo cha afya cha karibu, wengi wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita nne kutafuta matibabu. Wengine hulazimika kuvuka hadi wadi jirani ili kupata huduma.
Fikiria mama mjamzito aliye karibu kujifungua, au mzee anayeumwa ghafla hizi si hadithi za hekaya, bali ni hali halisi inayowakumba wakaazi kila siku. Kutokana na umbali mrefu, baadhi ya watu hulazimika kutibiwa katika hospitali za binafsi, jambo linalowagharimu pesa ambazo hawana. Lakini je, hali hii inafaa kuwa hivyo kweli?
Katika Mpango wa Maendeleo wa Mwaka wa 2022/2023, Zahanati ya Kambi Thomas ilitengewa shilingi milioni tatu nukta tano. Fedha hizi zilipaswa kutumika kuanza ujenzi wa kituo hicho ili kuleta huduma za afya karibu na wananchi. Leo, miaka mitatu baadaye, kinachoonekana ni msingi tu wa jengo hakuna ukuta, hakuna paa, hakuna huduma. Ni uwanja mtupu na ahadi zisizotimizwa.
Zahanati hii ingehudumia maelfu ya wakaazi, lakini mpaka sasa hakuna hatua kubwa iliyopigwa.
Wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika hivi karibuni katika Ofisi ya Chifu mkutano ulihudhuriwa na Mbunge wa eneo hilo, Bi Janet wakaazi walitoa malalamiko yao kwa mara nyingine. Wamechoka kungoja.
Mama Ruth, mjamzito kutoka Keroka, alisema kwa uchungu. “Lazima nipange siku kadhaa kabla ili nifike kliniki. Vipi kama uchungu wa kujifungua utaanza usiku? Vipi kama hakuna usafiri wa kufika mbali?.”
Mzee Kiptoo, mkaazi wa miaka mingi alisema kuwa yeye ana matatizo ya shinikizo la damu kisha akaongezea kusema “Siku nyingine nilitembea zaidi ya saa moja kwenda kupimwa shinikizo. Kufika huko nilikuwa hoi. Hii siyo haki kwa wananchi.”
Haya si matukio ya mtu mmoja mmoja ni sauti za mamia ya watu wanaoteseka kimya kimya ambao walionekana wakichangia sana na kuwapigia makofi watu ambao walileta malalamishi yanayowahusu.
Kwa mujibu wa Ibara ya 43(1)(a) ya Katiba ya Kenya ya 2010,
“Kila mtu ana haki ya kupata kiwango cha juu zaidi cha afya, ikiwemo huduma za afya.” Haki hii kwa sasa inakandamizwa.
MCA na viongozi wengine wa eneo hili hawapaswi kukaa kimya. Hili sio suala la majengo tu ni suala la maisha ya watu. Wakaazi wa Kapchumba hawaombi mengi. Wanaomba kile kilichopangwa, kilichotengewa pesa, na kilichoahidiwa.
Wakaazi wanahitaji huduma za afya sasa, si kesho, si baadaye.
Wakaazi hawajasahau. Wakaazi wako macho wanangojea.