Imeandikwa na Ahmed Karama
Nchi ya Kenya ni moja ya mataifa ambayo yamebarikiwa na milima maarufu ulimwenguni ambayo ni moja ya vivutio vikubwa vya utalii. Kaunti ya lamu nayo haijasazwa katika baraka hizi kwa sababu ni moja ya kaunti inayotegemea na inayopokea watalii wengi kwa sababu ya mandhari ya kipekee yenye kuwavutia watalii kutoka kote ulimwenguni ila utupaji ovyo ovyo wa takataka unatishia fahari hii ya lamu.
Maeneo mengine nchini Kenya wakijivunia kwa kubarikiwa na milima kama vile mlima Kenya, mlima Elgon nakadhalika, kaunti ya lamu tunajidhalilisha kwa kubarikiwa na milima ya taka ambayo ni tishio kwa sekta ya utalii.
Kaunti ya lamu ni moja ya maeneo ya kipekee nchini Kenya yanayojulikana kwa urithi wa kitamaduni, historia tajiri na vivutio vya utalii. Hata hivyo kwa miaka ya hivi karibuni lamu imekumbwa na changamoto ya taka, hasa kutokana na ongezeko la idadi ya watu, ukuaji wa mji na idadi kubwa ya watalii wanaotembelea eneo hili. Tatizo la usimamizi wa taka sasa limegeuka kuwa jinamizi na tishio kwa kwa afya ya wakaazi, ustawi wa mazingira na sura ya Lamu kama kivutio cha utalii.
Changamoto kubwa ni kuwa takataka hazikusanywi, kuchakatwa na kuondolewa majaani kwa muda ufaao hivyo basi taka nyingi hasa plastiki huishia baharini na kuhatarisha uhai wa viumbe wa baharini kama kasa, samaki na korali.
Sekta ya utalii na bahari ndio vinegar uchumi vikubwa katika kaunti ya lamu. Wageni hutegemea lamu kama eneo safi na lenye mandhari ya kuvutia lakini taka sokoni na mitaani huathiri taswira hiyo.
Je wa kulaumiwa ni serikali, jamii ama wanamazingira? Tatizo la taka Lamu limesababishwa na ukosefu wa mfumo thabiti wa ukusanyaji na uteketezaji wa taka, uelewa mdogo wa jamii kuhusu athari za utupaji taka ovyo na upungufu wa mapipa na magari ya taka na ukosefu wa ushirikiano baina ya jamii, serikali ya kaunti na wadau wa mazingira hivyo basi Kuna uzembe pande zote.
Changamoto ya taka katika kaunti ya lamu ni suala la kijamii, kiafya na kiuchumi. Suluhisho lake linahitaji mshikamano wa jamii, serikali ya kaunti na washikadau wa mazingira. Ikiwa hatua madhubuti zitachukuliwa, Lamu inaweza kuhifadhi haiba yake kama urithi wa dunia na kivutio cha kipekee cha watalii huku wakazi wakifurahia maisha katika mazingira safi na salama.