WritAfrica

MIAKA SITINI YA UHURU BILA NURU

IMEANDIKWA NA AHMED KARAMA 

Ni zaidi ya miaka sitini sasa tangu Kenya ipate uhuru, lakini hali ya upatikanaji wa umeme katika eneo la Lamu Mashariki bado ni duni na ya kusikitisha. Wakaazi wa maeneo kama Kiunga, Ishakani, Ndau, na Kizingitini wameendelea kuishi gizani, huku wakiendelea kulalamikia huduma duni ya usambazaji wa umeme inayotolewa kwa vipindi visivyotabirika.

Kwa muda wa miongo zaidi ya sita, wakazi wa lamu mashariki (kiunga, ishakani, ndau) wamekuwa wakitegemea umeme wa jenereta unaowashwa kwa muda mfupi, mara nyingi saa chache tu kwa siku, na wakati mwingine hakuna kabisa, hali ambayo imeathiri pakubwa shughuli  za kiuchumi, hasa sekta ya uvuvi ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi eneo hili.

Wananchi wa maeneo haya wanategemea samaki kwa maisha yao, lakini bila umeme, samaki wanaharibika kabla hata kufika sokoni. Wavuvi hukadiria hasara kubwa kila mara  kwa sababu hawawezi kugandisha samaki au kuhifadhi kwenye baridi, ila hali hii inaonekana kufumbiwa macho.

Tatizo la umeme limekuwa na athari kubwa si kwa wafanyabiashara wa barafu, si wachuuzi wa vyakula, na hata shule pia zimeathirika. Shughuli kama vile uchapishaji, matumizi ya mitambo ya kisasa, na hata masomo ya usiku yamesimama kutokana na ukosefu wa umeme wa uhakika.  Kulingana na Fatuma Ali ambae ni mkazi wa ishakani, wanafunzi wanalazimika kusoma kwa kutumia taa za mafuta au mishumaa, hali inayowaweka hatarini kiafya na kudidimiza maendeleo yao ya kielimu.

“Hata tukiwa na sola, haiwezi kuhimili matumizi ya kawaida. Friji hatuwezi kutumia, watoto wanashindwa kusoma usiku, na biashara nyingi zinakufa. Tumezoea giza hadi imekuwa kama sehemu ya maisha.”

Ahadi nyingi zimekuwa zikitolewa na viongozi wa serikali kuhusu kuimarishwa kwa miundombinu ya umeme, lakini hadi sasa hakuna mabadiliko yanayoonekana, ni miaka sitini ya ahadi zisizotekelezwa, watu bado wako gizani. Mohammed Bwana ambaye ni mkaazi wa kiunga anasema ahadi hewa zinazotolewa kila kukicha bila kutekelezwa zinawafanya wabaki nyuma kimaendeleo na kujihisi kama wanyonge waliotengwa. “Tumechoka kuahidiwa kila mwaka. Tunataka tuwe kama wenzetu sehemu nyingine za Kenya. Umeme ni haki, si zawadi. Bila umeme hatuwezi kusonga mbele.”

Ukosefu wa umeme wa uhakika ni kikwazo kikubwa kwa ustawi wa kijamii na kiuchumi wa Lamu Mashariki. Umeme ni nguzo muhimu ya maendeleo — unahamasisha uwekezaji, unarahisisha biashara, na unaleta teknolojia vijijini. Bila umeme, wakazi wanabaki nyuma katika nyanja zote za maendeleo.

Penye nia njia hupatikana, kinachohitajika ni serikali, viongozi na wawekezaji kushirikiana kwa pamoja ili kupatikane suluhisho la kudumu la suala la umeme lamu mashariki. Ni juhudi kidogo tu zinazohitajika ili wakaazi wa lamu mashariki waweze kuona nuru baada ya miaka mingi ya giza.

Tags:

No tags assigned to this post.

Related Posts

Top Categories

Trending News

False Accusers
Station Magistrates
The Rogue Officers
The Untouchable Estate Don
Kibuye Market Saga
 System Down: Patient Dead

Subscribe to Our Newsletter

Join our vibrant community of young poets, writers, and illustrators.