Imeandikwa na Ahmed Karama
Suala la unyakuzi wa ardhi katika kaunti ya lamu limekuwa donda sugu. Si suala lililoanza jana wala juzi bali ni suala nyeti la miaka na mikaka, kisa cha hivi karibuni kikiwa ni unyakuzi wa ardhi za shela. Vilio vya watu wa lamu wenye kudhulumiwa haki zao vimekuwa vikiangukia katika sikio la kufa ambalo halisikii dawa. Wanasiasa wenye ushawishi serikalini na mabwenyenye wenye senti zao wamekuwa wakitumia maguvu yao na kuthibitisha maana halisi ya methali ‘mwenye nguvu mpishe’
Eneo la shela kisiwani amu ni eneo tajika ulimwenguni kote kwa mandhari yake murua ya kupendeza na kuvutia watalii kutoka pande zote za ulimwengu si mashariki si magharibi. Kivutio kikubwa ambacho kinaifanya shela iwe na mvuto wa kipekee ni matuta ya michanga (sand dunes) yanayopatikana katika ufuo wa bahari ambayo yana umuhimu mkubwa kwa viumbe hai wa ardhini na majini ila kuna baadhi ya wafisadi wenye matumbo yasiyoshiba wanaoona matumbo yao ni muhimu kuliko maslahi ya wanashela na viumbe wa baharini kama kasa.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na njama ya kunyakuwa baadhi ya ardhi eneo la shela hususan upande wa milima ya michanga. Unyakuzi wa ardhi hii ni hatari si kwa binadamu pekee bali pia kwa viumbe wa baharini.
Katika eneo hili ndipo zinapopatikana chemichemi na visima vya maji vinavyotumika kusambaza maji katika kisiwa kizima cha lamu, maji ambayo tayari hayatoshi. Je eneo hili likinyakuliwa hali ya wakaazi wa lamu itakuwaje?
Sehemu hii pia ndio pahali panapotumiwa na viumbe wa baharini kama kasa kutaga mayai yao nyakati za usiku hivyo basi kuwepo kwa kasa ambao ni nadra sana kupatikana hivyo basi tamaa ya mabwenyenye hawa inatishia pia kupungua na kupotea kabisa kwa viumbe hawa muhimu kwa utalii wa lamu.
Ripoti zinaonyesha kuwa baadhi ya watu wenye ushawishi wamekuwa wakitumia mbinu za hila kujipatia vipande vya ardhi shela. Hali hii inatishia sio tu ustawi wa wananchi bali pia mazingira na urithi wa kitamaduni unaotambulika kitaifa na kimataifa.
Wataalamu wa mazingira wameonya kuwa iwapo hali hii haitashughulikiwa mapema, lamu inaweza kupoteza sifa yake ya kipekee kama ngome ya turathi za dunia na makazi ya jamii zilizoishi lamu kwa karne nyingi. Unyakuzi wa ardhi shela ni kikwazo kikubwa kwa ustawi wa jamii, uhifadhi wa mazingira na urithi wa kitamaduni wa lamu. Ni jukumu la washikadau wote kuhakikisha kuwa mali ya umma inalindwa dhidi ya walafi wachache.
Kuilinda shela ni kulinda mustakabali wa vizazi vijavyo.