IMEANDIKWA NA AHMED KARAMA
Tamasha za kuonyesha utamaduni wa Lamu zimekuwa kivutio kikubwa kila mwaka, zikiwaleta pamoja wageni kutoka pembe zote za nchi na hata mataifa ya mbali. Wiki iliyopita, shamrashamra hizi zilimalizika kwa mafanikio makubwa, huku wageni wakipata fursa ya kushuhudia utajiri wa utamaduni wa Waswahili, uzuri wa ufundi, muziki, ngoma na mashindano ya jahazi ambayo huipa Lamu utambulisho wa kipekee. Hata hivyo, nyuma ya mandhari hayo ya kuvutia, kulibainika changamoto kubwa ya uchafuzi wa bahari.
Katika kipindi cha tamasha, bahari ya Lamu ilionekana kuwa chafu zaidi kuliko kawaida. Chupa za plastiki, makopo, mifuko, na taka nyingine za plastiki zilikuwa zikielea juu ya maji au kutapakaa katika ufukwe. Hali hii haikuharibu uzuri wa bahari pekee, bali pia iliibua shaka kubwa kuhusu mustakabali wa mazingira ya baharini, afya ya viumbe maji, na taswira ya Lamu kama kivutio cha utalii.
Serikali ya kaunti ya lamu kupitia kwa kamati husika ya kupanga tamasha za utamaduni wanahitaji kutambua kuwa wakati huu huwa na ongezeko la watu waliofurika kushuhudia tamaduni za lamu hivyo basi kueka mikakati na mifumo kamili ya kukusanya na kutupa chupa za plastiki pamoja na aina mbalimbali za takataka ili kulinda mazingira yetu na hadhi ya lamu kama kituo kikubwa cha utalii Kenya.
Athari za uchafuzi huu ni kubwa na zenye kuumiza hata viumbe wa baharini. Bahari ya Lamu ni makazi ya viumbe muhimu kama kasa, samaki na matumbawe, ambavyo ni sehemu ya mfumo wa ikolojia wenye umuhimu mkubwa kwa uchumi na utalii. Vipande vya plastiki huweza kumezwa na viumbe hawa, na hivyo kusababisha vifo, magonjwa, au kupungua kwa idadi yao. Uchafuzi huo pia huathiri wavuvi wa Lamu wanaotegemea bahari kwa riziki zao, kwa kuwa kupungua kwa viumbe maji kunaweza kupunguza mavuno ya samaki.
Aidha, utalii ambao ni uti wa mgongo wa uchumi wa Lamu unaweza kudorora kutokana na mandhari machafu. Wageni wengi husafiri Lamu kwa ajili ya kufurahia utulivu, uzuri wa bahari safi na mazingira ya asili. Hali ya bahari chafu inaweza kuwakatisha tamaa kurejea, na hivyo kupunguza mapato ya jamii.
Ni rahisi kuwanyooshea kidole cha lawama serikali ya kaunti ila ukweli ni kuwa ili kukabiliana na changamoto hii, ushirikiano unahitajika kati yao, wenyeji, wafanyabiashara na wageni. Kwanza, ni muhimu kuongeza vituo vya kutupa taka hasa katika maeneo yenye shughuli nyingi za tamasha. Pili, kampeni za uhamasishaji kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira zinapaswa kuimarishwa kabla, wakati na baada ya tamasha. Tatu, adhabu kali zinapaswa kutolewa kwa watakaokiuka sheria za mazingira, ili kuzuia tabia ya kutupa taka hovyo. Hatua nyingine ni kuhimiza matumizi ya chupa zinazoweza kutumiwa tena badala ya plastiki za kutupa.
Kwa pamoja, hatua hizi zinaweza kuifanya Lamu kudumisha hadhi yake kama miongoni mwa maeneo bora ya utalii nchini Kenya. Bahari safi ni urithi wa thamani ambao tunapaswa kuulinda kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Tamasha hupita, lakini mazingira hubaki, ni jukumu letu kuhakikisha tunayaacha katika hali bora.
