IMEANDIKWA NA AHMED KARAMA
Kwa muda mrefu sasa, Lamu imekuwa ikikabiliwa na matatizo mengi ya msingi kama ukosefu wa maji safi, huduma duni za afya, miundombinu mibovu, usalama mdogo wa chakula, gharama ya juu ya maisha na ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana. Kutokana na changamoto hizi ni matumaini ya wengi kuwa fedha nyingi za miradi zitaelekezwa kutatua matatizo nyeti ya wakaazi wa lamu ila cha kushangaza hali ni tofauti kabisa wengi wakijiuliza ikiwa serikali ya kaunti inafuatilia mahitaji halisi ya wananchi wake.
Katika mwaka wa kifedha wa 2023-2024 serikali ya kaunti ya lamu ilitumia takriban shilingi milioni 6.4 kujenga vibaraza viwili katika maeneo ya ufuo wa pwani kwa nia ya kutoa sehemu za kupumzikia na kubarizi kwa wakazi na watalii jambo ambalo limezua mjadala mkali miongoni mwa wakaazi na wadau wa maendeleo. Baadhi ya viongozi wa kijamii na wananchi wa kawaida wameutaja mradi huu kama “kipaumbele kisicholingana na mahitaji halisi ya wananchi.”
Katika maeneo kama Lamu Mashariki, Kiunga, Kizingitini, na hata sehemu za Lamu Magharibi, wananchi bado wanakumbwa na tatizo la uhaba wa maji, huku wengine wakitegemea visima vya kienyeji ambavyo mara nyingi si salama kwa matumizi. Wengine wanahangaika kupata huduma muhimu kama dawa, wazazi wakijikuta wakitembea kilomita nyingi kuwapeleka watoto hospitali kutokana na ukosefu wa vituo vya afya vilivyo na vifaa vya kutosha. Wakulima na wavuvi pia wanasema wanahitaji uwekezaji katika miradi ya uzalishaji, si mandhari pekee.
Katika maeneo kama Kiunga, Kizingitini, na baadhi ya sehemu za Mpeketoni, wananchi wanalia ukosefu wa hospitali zenye vifaa, barabara zisizopitika wakati wa mvua, na changamoto za elimu. Kwao, matumizi ya mamilioni ya pesa kwa miundo ya kupumzikia yanaonekana kama ishara ya ukosefu wa uongozi unaoangalia mahitaji ya wengi.
Kulingana na mama Amina ambae ni mkaazi wa langoni anasema “Tunashangaa kuona kaunti inajenga vibaraza wakati bado tuna tatizo la uhaba wa maji ya kunywa. Kipaumbele hiki hakilingani na hali halisi. Maendeleo si mapambo—ni huduma za msingi.”
Aidha mzee fadhili ambae ni mfanyibiashara mjini lamu ameshadidia nukta hii na kusema “Sio vibaya kuwa na vibaraza, lakini si wakati huu. Miaka nenda miaka rudi tunalilia maji, hospitali na barabara. Lazima kipaumbele kiwekwe pale wananchi wanapoteseka zaidi.”
Hata hivyo, wapo wanaotetea mradi huo wakisema unaweza kuongeza uzuri wa mji wa kale wa Lamu, kuvutia watalii zaidi na kuboresha biashara za ufukweni kama vile uuzaji wa vyakula, sanaa na utamaduni ila mafanikio hayo hayapaswi kuja kwa gharama ya kupuuzia mahitaji ya msingi ya watu.
Matumizi ya milioni 6.4 kujenga vibaraza kwenye ufuo ni somo muhimu kuhusu uhitaji wa kupanga maendeleo kwa kuzingatia mahitaji halisi. Wananchi wa Lamu wanahitaji kuona kwamba rasilimali zao zinatumika kwa busara, uwazi na kwa manufaa ya wengi, si kwa miradi ya kupendeza macho bila kuleta mabadiliko ya kimsingi katika maisha yao.
Ni wakati wa viongozi kutafakari kwa kina kuhusu vipaumbele vya kaunti—kwa sababu maendeleo ya kweli hayapimwi kwa uzuri wa mandhari pekee, bali kwa huduma bora, maisha salama, na ustawi wa watu wake.
