WritAfrica

KENYA KWENYE MIZANI

Imeandikwa na Ahmed Karama 

Dunia ya sasa imejaa changamoto ambazo zimevuruga maisha ya kawaida.  Changamoto hizi zimeifanya dunia ionekane kama haieleweki tena na hakuna uhakika wa kesho. Kenya ni moja ya mataifa  yanayotajika kwa kuongoza kwa demokrasia lakini tujiulize hii demokrasia nini?  Inaumiza kuona kuwa kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa demokrasia na uzalendo ni kuenda kupiga kura tu, wasichofahamu ni kuwa demokrasia ni uwanja mpana ambao hata wataalamu hawajaweza kuuchanganua kikamilifu. Lau utachukua wataalamu japo watatu uwaulize swali moja tu, demokrasia ni nini basi nina uhakika majibu yao hayataoana, thibitisho tosha kuwa demokrasia ni uwanja mpana na kila mmoja anaufahamu wake wa uwanja huu. 

Demokrasia si kura  bali ni kuhakikisha kuwa watu wote wana nafasi ya kushiriki na kusikilizwa kikamilifu, si vijana si wazee, si wanawake si wanaume, si maskini si tajiri, si wachache si wengi, si wagonjwa si wazima. Demokrasia ni kuhakikisha wote wanahusishwa na hawabaguliwi. 

Wakati wa hofu na changamoto mara  nyingi haki za watu hukiukwa, hukandamizwa na sauti zao kupuuzwa. Tunakabiliana na nyakati ngumu na mashaka, wengi wakiteseka na ukosefu wa kazi, wakiogopa kwa kukosekana haki, ukandamizaji wa kisiasa na hata majanga ya asili. Wasiwasi huu unasababisha baadhi ya serikali kupuuza uhuru wa raia au kutojali haki zao.

Demokrasia na usalama ni nyanja mbili ambazo huenda pamoja kwa karibu. Demokrasia haiwezi kustawi katika mazingira yenye ukosefu wa usalama, na vivyo hivyo, usalama hudumishwa vyema zaidi pale ambapo misingi ya kidemokrasia kama haki za binadamu, utawala wa sheria, na usawa vinaheshimiwa. Nchini Kenya, usalama umekuwa kipimo muhimu cha ubora wa demokrasia, hasa kutokana na changamoto za maandamano ya kisiasa, na mivutano ya kikabila.

Mara nyingi maandamano ya kisiasa hutazamwa kama sehemu ya demokrasia. Hata hivyo, kukabiliana na maandamano hayo kumekuwa kukihusisha matumizi ya nguvu kupita kiasi na kusababisha migongano kati ya wananchi na vyombo vya dola.

 Serikali wamekuwa wakishutumiwa vikali kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji ambao wamekuwa wakitetea haki zao za kimsingi. Wengi wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya baina ya mwaka jana na mwaka huu yote yakianzia na maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka elfu mbili ishirini na nne/ishirini na tano. Licha ya masaibu hayo kutokea mpaka sasa serikali ya Kenya imekaa kimya, wanajifanya hawaoni wala hawasikii. Waathiriwa wakiuguza majeraha, na wengine wakilala usingizi wa milele, wahalifu waliotenda maovu haya wapo mitaani wanatembea huru. Cha kuliza ni kuwa serikali imesema itawafidia waathiriwa, je hii ndio haki ya nchi ya demokrasia?

Ni muhimu tujiulize je demokrasia itaendelea kudumu vipi katika nchi yenye vurugu na changamoto chungu nzima? Na je tunawezaje kuhakikisha kila mtu anajumuishwa na kusikizwa, hata katika nyakati za hofu na misukosuko? Na je vijana na jamii wanawezaje kulinda haki na thamani za kidemokrasia wakati dunia imejaa wasi wasi? Tukipata majibu ya maswali haya basi demokrasia yetu itakuwa imekamilika.

Demokrasia nchini Kenya ni mchakato unaoendelea badala ya kuwa hali iliyokamilika. Licha ya changamoto za ukabila, rushwa, na matumizi ya nguvu kupita kiasi, hatua kubwa zimepigwa katika kukuza haki za raia, uwajibikaji, na ushiriki wa wananchi kupitia ugatuzi. Ili kuimarisha zaidi demokrasia, ni muhimu kuimarisha taasisi huru, kupambana na ufisadi, na kuendeleza mshikamano wa kitaifa unaozingatia maslahi ya wote bila misingi ya kikabila. Hatua hizi zitahakikisha kuwa demokrasia ya Kenya inakuwa ya kweli, shirikishi na endelevu.

Dunia ya sasa imevurugika na kuna hofu nyingi lakini bado ni muhimu demokrasia ibaki imara na ijumuishwe kwa wote

Tags:

No tags assigned to this post.

Related Posts

Top Categories

Trending News

You Know We are Kin, I and You
The People’s Peace
Siasa Ya ID
UFISADI TIA  ZII
HEALTH SERVICE CHRONICLES
Protest is Not A Crime - Article 37

Subscribe to Our Newsletter

Join our vibrant community of young poets, writers, and illustrators.