IMEANDIKWA NA AHMED KARAMA
Katika mji wa Lamu, suala la uchimbaji holela wa mashimo ya choo na visima limekuwa tatizo sugu linaloakisi pengo kubwa katika usimamizi wa mazingira na afya ya jamii. Tabia hii imeenea katika maeneo mengi ya makazi, ambako mashimo ya choo na visima huchimbwa katikati ya barabara au moja kwa moja nje ya nyumba, sehemu ambazo watu hupita kila siku na watoto hucheza bila kujua hatari inayowakabili. Hali hii imezua maswali mazito miongoni mwa wakaazi: Je, wahusika wa kusimamia na kufuatilia masuala haya wako wapi?
Kwa mujibu wa miongozo ya afya ya mazingira, umbali kati ya shimo la choo na kisima unapaswa kuwa kati ya mita 15 hadi 30 ili kuzuia uchafuzi wa maji ya matumizi. Hata hivyo, sheria hii muhimu haifuatwi kabisa katika sehemu nyingi za Lamu. Watu huchimba mashimo kwa kuzingatia nafasi inayopatikana, si kwa kutanguliza usalama wa afya ya jamii. Matokeo yake, maji mengi ya visima yameendelea kukumbwa na uchafuzi, jambo linaloongeza hatari ya magonjwa kama kuhara, kipindupindu, homa ya matumbo na maambukizi mengine yanayotokana na matumizi ya maji machafu.
Katika mazingira kama ya Lamu ambako watu wengi hutegemea visima kama chanzo kikuu cha maji, athari za uchimbaji holela wa mashimo ya choo ni kubwa. Lamu ni sehemu ambayo ardhi yake ni ya mchanga laini hivyo basi uchafu hutiririka kwa urahisi na kufikia visima vilivyo karibu. Wakaazi wengi wanasema kuwa maji yao mara nyingi huwa na harufu isiyo ya kawaida au hubadilika rangi, ishara ya uwezekano mkubwa wa uchafuzi.
Lakini athari hizi si za kiafya pekee. Mashimo ya choo na visima yaliyopo barabarani pia yanaweka watu kwenye hatari ya kupata majeraha au hata kupoteza maisha. Wazazi wengi wanasema wamekuwa wakiishi kwa hofu kila siku watoto wanapocheza mitaani. Mashimo mengi hufunikwa kwa mbao dhaifu au magogo ambayo huweza kupasuka muda wowote, na kusababisha mtu kudondoka ndani. Ni jambo la kushangaza kwamba katika mji ulioorodheshwa kama urithi wa dunia (UNESCO World Heritage Site), bado kuna ukosefu mkubwa wa mipangilio ya msingi ya kimazingira.
Halmashauri za mitaa kupitia idara ya afya na mazingira zinapaswa kuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba ujenzi wa mashimo ya choo na visima unafuata viwango vinavyokubalika. Hata hivyo, hili halifanyiki. Maafisa wanaotakiwa kufuatilia na kutoa maelekezo kuhusiana na sheria zilizowekwa mara nyingi hawafiki katika maeneo husika na kuishia kutoa maagizo bila kufuatilia utekelezaji wake. Hali hii imewafanya baadhi ya watu kuchukulia suala la usafi kama jambo la hiari badala ya wajibu wa lazima kwa afya ya jamii nzima.
Je jamii ya lamu wanapaswa kulaumiwa kutokana na utepetevu huu? Jibu ni ndio, tunaweza kuwalaumu au la tusiwalaumu. Ukosefu wa elimu ya afya ya mazingira kwa wananchi umechangia kwa kiwango kikubwa kuongezeka kwa tatizo hili. Watu wengi hawajui madhara ya uchafuzi wa maji, wala hawafahamu umuhimu wa kufuata umbali unaotakiwa kati ya shimo la choo na kisima. Kampeni za uhamasishaji zinazotolewa na serikali au mashirika binafsi zimekuwa hafifu, na nyingi hufanyika mara chache bila kufuatiliwa kwa vitendo.
Kuna haja ya utaratibu mkali wa ukaguzi wa maeneo ya makazi, hasa katika sehemu zenye msongamano mkubwa. Jamii inapaswa kuhamasishwa kuhusu umuhimu wa usafi na madhara ya uchafuzi wa maji yanayotokana na uchimbaji holela. Viongozi wa kijamii, wazee wa mtaa, na mashirika ya afya wana jukumu kubwa la kuelimisha wananchi na kusimamia utekelezaji wa sheria ndogondogo za usafi.
Katika karne hii ambapo afya ya jamii ni msingi wa maendeleo, ni muhimu kwa serikali kuhakikisha kwamba usalama wa wananchi unatangulizwa. Mashimo ya choo na visima havipaswi kuwa chanzo cha hofu au magonjwa, bali yatumiwe kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazolinda ustawi wa jamii yote ya Lamu.
Kwa mji unaotegemea utalii na unaojivunia historia ndefu, ni jambo la aibu kwamba masuala ya kimsingi kama usimamizi wa uchafu bado ni changamoto.
