Imeandikwa na Alex Maina
Barabara ya Kambi Teso hadi Bondeni ni kama uti wa mgongo wa wakazi wa maeneo haya. Ni njia muhimu sana inayounganisha wakazi wa Upper Bondeni, Lower Bondeni, na Kambi Teso na mji wa Kamukunji. Ni kupitia barabara hii ndipo watu huenda kazini, watoto hushika njia ya shule, kina mama hupeleka bidhaa sokoni, na wagonjwa hufika hospitalini.
Kwao, hii si barabara tu ni sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Lakini sasa barabara hii imegeuka kuwa chanzo cha mateso makubwa.
Mvua inaponyesha, barabara hubadilika kuwa mteremko wa matope. Mashimo hujaa maji na hakuna anayepita bila kuteleza au kuchafuka. Watoto wakitoka shule hulazimika kuvua viatu ili wavuke. Kina mama wakitoka sokoni hujikwaa, na mizigo yao hutapakaa chini.
Wakati wa Kiangazi, hali huwa mbaya zaidi kwa njia nyingine. Vumbi hufunika kila kitu. Chakula ndani ya nyumba hujaa vumbi. Watoto hupumua hewa chafu. Watu hufungwa macho kwa sababu ya vumbi kali. Magonjwa ya mapafu na mafua yamekuwa ya kawaida.
Mzee Kamau, mkazi wa Upper Bondeni, anasema kwa uchungu, “Hii barabara tumekuwa tukilalamika miaka mingi. Tulinyamaza tukingoja mabadiliko. Lakini sasa ni wazi hakuna anayetusikia. Tunahitaji barabara hii ijengwe sawasawa.”
Mama Sarah kutoka Kambi Teso anaongeza, “Mara ya mwisho nilijaribu kupeleka mtoto hospitali usiku, pikipiki iligoma. Mvua ilikuwa imenyesha, njia ilikuwa matope tupu na hata pia kupata gari ata ya Jirani ilikua kizungumkuti. Tulingojea hadi asubuhi ndo tuweze kukimbia hospital”
Barabara hii inasababisha ucheleweshaji, ajali ndogo ndogo, na magonjwa. Inavunja ndoto za watoto, na kuwatesa wakazi kila siku.
Wakaazi wa Kambi Teso na Bondeni wanatoa wito kwa Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu kuchukua hatua za haraka. Wanataka barabara ya kudumu, si ya muda mfupi. Sio tena kuweka kifusi au kusawazisha udongo bali kujenga barabara imara, yenye mifereji na inayopitika kila siku ya mwaka.
Hawa wakazi hawadai mambo makubwa. Wanataka tu mazingira salama ya kuishi na kusafiri. Wanataka hadhi kama ya wakaazi wa maeneo mengine ya kaunti. Wanataka watoto wao wasichelewe shule, wagonjwa wafike hospitali kwa wakati, na kina mama wawe na amani wakitafuta riziki.
Ni wakati wa kusikia kilio cha watu wa Kambi Teso na Bondeni. Ni wakati wa kujenga barabara ya matumaini.
