IMEANDIKWA NA AHMED KARAMA
Zahanati ya Wiyoni, moja ya vituo muhimu vya afya vilivyoko katika kaunti ya Lamu, imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ambazo zimeathiri utoaji bora wa huduma za afya kwa wakazi wa eneo hilo. Pamoja na kuwa tegemeo kuu kwa wakazi wa Wiyoni na vitongoji vyake, zahanati hiyo inakabiliwa na hali ngumu inayohitaji kuingiliwa kati haraka iwezekanavyo kutoka kwa serikali na wadau wa afya ili kuhakikisha huduma bora zinarejea.
Changamoto kubwa zaidi inayokikumba kituo hicho ni uhaba wa wahudumu wa afya. Kwa sasa, zahanati hiyo inahudumiwa na wahudumu wachache ambao wanalazimika kufanya kazi kwa muda mrefu bila mapumziko ya kutosha. Wakati mwingine, wagonjwa wanafika kupata huduma lakini hukosa daktari au muuguzi wa kuwahudumia kwa sababu wahudumu wachache waliopo hushughulika na wagonjwa wengi kwa wakati mmoja. Hali hii imepelekea ucheleweshaji wa matibabu, huku wagonjwa wengine wakilazimika kutafuta huduma za matibabu katika hospitali za kibinafsi ili kupata huduma bora zaidi.
Zaidi ya hayo, uhaba wa vifaa vya tiba ni tatizo lingine linaloikumba zahanati hiyo. Vifaa kama vile mashine za kupima shinikizo la damu, vifaa vya kujifungulia akina mama, dawa muhimu, na vifaa vya maabara havipatikani kwa wingi. Hii imeathiri kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma za dharura, hasa kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa haraka. Mara nyingine, wagonjwa hulazimika kununua dawa kutoka maduka binafsi, jambo ambalo huongeza mzigo wa kifedha kwa familia maskini.
Changamoto nyingine kubwa ni uhaba wa usalama. Inashangaza kuona kuwa zahanati ya Wiyoni inategemea mlinzi mmoja pekee, ambaye akipatwa na dharura au kutohudhuria kazini, kituo hubaki bila ulinzi kabisa. Hali hii inahatarisha usalama wa vifaa vilivyomo ndani ya kituo, na pia usalama wa wagonjwa na wahudumu. Usiku, zahanati inakuwa katika hatari kubwa ya wizi au uhalifu, jambo linalozua wasiwasi kwa watumishi na wakazi wanaohitaji huduma za dharura nyakati hizo.
Wakazi wa Wiyoni wamekuwa wakitoa wito kwa serikali ya kaunti ya Lamu kupitia idara ya afya kuingilia kati kwa kuongeza wahudumu, kuboresha miundombinu, na kuhakikisha usalama wa kituo hicho. Wanasisitiza kuwa afya ni haki ya kimsingi kwa kila mwananchi kama inavyoelezwa katika Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, hivyo serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha zahanati hiyo inafanya kazi ipasavyo.
Zahanati ya Wiyoni ni kielelezo cha matatizo yanayovikumba vituo vingi vya afya lamu. Bila uwekezaji wa kutosha katika sekta ya afya, wananchi wataendelea kuteseka na kukosa huduma bora wanazostahili. Ipo haja ya washikadau wote, wakiongozwa na serikali ya kaunti na jamii yenyewe, washirikiane kuinua hali ya afya katika maeneo kama Wiyoni.
Tusipoziba ufa, tutajenga ukuta.
