IMEANDIKWA NA AHMED KARAMA
Kwa miaka mingi tangu kuzinduliwa kwa vituo vya Huduma Centre nchini Kenya, maeneo mengi ya mijini na vijijini yamepata fursa ya karibu ya kufikia huduma za serikali. Hata hivyo, hali hiyo haijawafikia wakaazi wa Lamu Mashariki, jambo ambalo linazidi kuleta malalamiko na mateso kwa wakazi wa maeneo kama Kiunga, Ndau, Faza, Kizingitini, na Basuba.
Watu wa lamu mashariki wameteseka kwa muda mrefu katika juhudi za kutafuta huduma muhimu za serikali kama vile usajili wa vitambulisho, vyeti vya kuzaliwa, NSSF, SHIF, na huduma nyinginezo muhimu. Wakaazi wa maeneo haya hulazimika kusafiri masafa marefu hadi mjini lamu ili kupata huduma hizi muhimu.
Inawezekanaje mkenya anaelipa ushuru kutumia maelfu ya pesa kwa ajili ya kutafuta huduma muhimu za serikali? Je huu ni uungwana? Nauli pekee kutoka kiunga kufika hadi lamu inaweza kufika zaidi ya elfu tano, ukiongeza gharama ya malazi na chakula. Kwa sababu ya gharama nyingi wanazopitia watu wengi wanakata tamaa na kuishia kuishi bila stakabadhi muhimu za kiserikali.
Safari kutoka Lamu Mashariki hadi mjini Lamu si rahisi. Wakaazi hulazimika kutumia boti kwa saa kadhaa kupitia baharini, na hali mbaya ya hewa au upepo mkali hufanya safari hizo kuwa hatarishi. Kwa wanafunzi wanaohitaji vyeti vya kuzaliwa, vijana wanaotafuta ajira au wanaoomba huduma za serikali, changamoto hii imekuwa kikwazo kikubwa katika maendeleo yao.
Ukosefu wa kituo cha huduma za serikali ni ishara ya kutengwa kwa maeneo ya pembezoni kama Lamu Mashariki. Huduma za serikali zinapaswa kuwa za usawa na zipatikane kwa urahisi kwa wananchi wote, bila kujali umbali au jiografia ya eneo.
Huduma Centre ni mpango mzuri ulioanzishwa kwa lengo la kuleta huduma karibu na wananchi. Lakini sehemu kama Lamu Mashariki hazijanufaika, basi dhana ya ‘huduma kwa wote’ inakuwa haina maana.
Serikali ya kitaifa na serikali ya kaunti ya Lamu wanapaswa kushirikiana kuhakikisha Huduma Centre inajengwa Lamu Mashariki. Hatua hiyo itapunguza gharama, kuongeza ufanisi wa huduma, na kuboresha maisha ya wananchi wa lamu mashariki.
