IMEANDIKWA NA AHMED KARAMA
Kwa zaidi ya wiki mbili sasa, wakaazi wa mtaa wa Gardeni katika mji wa Lamu wamekuwa wakikumbwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji safi ya kutumia. Hali ambayo imewalazimu wakazi hao kutafuta mbinu mbadala ya kutafuta haki yao ya uhai, maana maji ni uhai. Kukosekana kwa maji siku moja ama mbili tu ni kero tosha kwa binadamu sembuse kukosekana kwa maji wiki mbili? Kinachoumiza kichwa zaidi ni ukimya unaoshuhudiwa kutoka kwa kampuni ya maji ya lamu, Lamu Water and Sewerage Company (LAWASCO).
Ukimya na kutowajibika kwa LAWASCO kumesababisha kero kubwa hasa kwa familia zenye watoto wadogo na watu wazima ambao hawawezi hata kujisaidia kujitafutia maji japo ya kuogea. Mzigo wao ukiwaangukia wachache wanaojiweza katika familia kuzunguka na mitungi ya maji wakitafuta maji japo ya matumizi nyumbani. Kwa upande wa maji ya kunywa, wengine wanalazimika kununua maji kutoka kwa wauzaji binafsi kwa bei ya juu, hali inayoongeza mzigo wa maisha kwa wananchi wa kipato cha chini.
Baadhi ya familia wanahofia afya zao baada ya kutumia maji kutoka kwa visima ambayo vinakaa muda mrefu bila kusafishwa wala kukaguliwa na kitengo cha afya ya umma ya jamii. Familia hizi wakigonjeka na maradhi ya tumbo ama kipindupindu nani atawajibika?
Licha ya tatizo hili kuwa nyeti, wakaazi wa gadeni hawajapokea taarifa yoyote rasmi kutoka LAWASCO. Kampuni ya LAWASCO wana jukumu la kueleza chanzo cha tatizo au hatua zinazochukuliwa kurejesha huduma hiyo muhimu ila ukimya wao unashutua. Ukimya huu umeibua hasira na taharuki miongoni mwa wakaazi, wakidai kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiwapuuzia kila mara kunapojitokeza hitilafu ya usambazaji wa maji.
Ukosefu wa maji unaweza kuathiri usafi wa mazingira na kutishia kutokea kwa hatari ya milipuko ya magonjwa yanayosababishwa na uchafu. Shughuli nyingi za nyumbani kama upishi, usafi na usafi wa mavazi zimesimama, hali inayodidimiza ubora wa maisha.
Wakazi wa Gardeni sasa wanaiomba serikali ya kaunti ya Lamu kuingilia kati na kushinikiza LAWASCO kurejesha huduma hiyo haraka iwezekanavyo. Wamesema maji ni haki ya msingi ya binadamu na hawapaswi kuachwa kuteseka bila suluhisho.
Kwa sasa, matumaini yao pekee ni kwamba kampuni husika itasikia kilio chao na kuchukua hatua za dharura kurejesha huduma hiyo muhimu, ili wakaazi wa Gardeni waendelee na maisha yao ya kila siku bila mateso.
Wakaazi wa gadeni, wana haki ya kupata maji safi haraka iwezekanavyo kama wengine wanyojivunia haki hiyo muhimu.
Maji ni haki ya msingi na maji ni uhai.
