WritAfrica

UHABA WA SHULE

Imeandikwa na Ahmed Karama 

Elimu ni haki ya msingi ya kila mtoto na nguzo muhimu ya maendeleo ya jamii na taifa. Taifa likitaka kuendelea lazima liwekeze vizuri katika sekta ya elimu. Katiba ya Kenya ya mwaka 2010 inatambua elimu kama haki ya kimsingi ya kila Mkenya. Ibara mbalimbali zimeeleza jukumu la serikali na haki za raia kuhusu elimu. Serikali ina jukumu la kuhakikisha watoto, vijana na hata watu wenye ulemavu wanapata elimu bila ubaguzi wowote. Licha ya kuwa serikali inajitahidi kulifanikisha hili, sekta hii inakumbwa na changamoto si haba, juhudi zaidi bado zinahitajika kuiboresha na kuitukuza elimu. Moja ya changamoto kubwa inayokumba elimu hususan kaunti ya lamu wadi ya mkomani ni uhaba wa shule.

 Kukosekana kwa shule za kutosha kunaathiri moja kwa moja upatikanaji  wa elimu bora lamu. Wadi nzima ya mkomani ambayo ina wapiga kura takriban 12,571 kulingana na takwimu za uchaguzi wa 2022, iko na shule mbili pekee za msingi, moja ikiwa no ya wasichana moja ni ya wavulana. Sasa ikiwa idadi ya wapiga kura ni hiyo tujiulize wanafunzi wanaotakiwa kuenda shule ni wangapi?

Wanafunzi hulazimika kutembea au kusafiri kwa muda mrefu kufika shuleni. Hii hupelekea uchovu, utoro, na wakati mwingine kuacha shule kabisa. Shule ya wavulana ya Mahmud bin Fadhil na Ile ya wasichana  zimekuwa zikikumbwa na  idadi kubwa ya wanafunzi, jambo linalosababisha walimu kushindwa kuwapa uangalizi wa kutosha wanafunzi. Shule hizi zimekuwa zikishuhudia msongamano wa wanafunzi na uhaba wa vifaa vya masomo vinavyoathiri ubora wa elimu na kusababisha matokeo duni ya mitihani.

Watoto wengi hasa wale wanaoishi mbali na shule hukata tamaa kwa sababu ya safari ndefu au mazingira magumu shuleni, na hatimaye kuacha shule. Watoto hawa wananyimwa nafasi sawa na wenzao kutoka maeneo mengine  hivyo basi  kuongeza pengo la kielimu. Watoto wa kike mara nyingi huathirika zaidi kwani wazazi huhofia kuwaacha watembee masafa marefu kwenda shule, hivyo kuongezeka kwa ndoa na mimba za mapema.

Licha ya wazazi na wadau wa elimu kulalamikia suala hili, bado hajiweza kutekelezwa. Ipo haja ya serikali kuweka mipango na mikakati kabambe ya kuongeza shule za umma hususan katika maeneo ambayo yanakuwa kwa kasi ya hali ya juu. Katiba ya Kenya inasisitiza kwamba elimu ni haki ya kimsingi, ni ya lazima na ya bure kwa shule za msingi, na serikali ina jukumu la kuhakikisha watoto, vijana na hata watu wenye ulemavu wanapata elimu bila ubaguzi wowote.

Tukumbuke asiyejua ni sawa na asiyeona hivyo basi watoto wanapaswa kupewa taa ya elimu yenye kuwaongoza gizani.

Kusoma ni kama kupanda mbegu, matunda yake huonekana baadae.

Tags:

No tags assigned to this post.

Related Posts

Top Categories

Trending News

You Know We are Kin, I and You
The People’s Peace
Siasa Ya ID
UFISADI TIA  ZII
HEALTH SERVICE CHRONICLES
Protest is Not A Crime - Article 37

Subscribe to Our Newsletter

Join our vibrant community of young poets, writers, and illustrators.