Imeandikwa na Ahmed Karama
Kaunti ya lamu inayojulikana kwa urithi wake wa kiswahili, miji ya kale yenye historia ndefu na vivutio vya kipekee vya asili kama fukwe safi, hifadhi za wanyamapori na mandhari ya kuvutia, imekuwa moja ya nguzo kuu za utalii nchini Kenya ila je serikali ya kaunti ya lamu wanatambua thamani ya sekta hii adhimu?
Mji wa kale wa lamu (old town) ni mojawapo ya miji ya kale zaidi na iliyohifadhiwa vyema mpaka kutambuliwa kama eneo la turathi ya ulimwengu wa UNESCO, kitu ambacho kimeifanya lamu kutambulika ulimwenguni na kuvutia watalii kutoka kote kuja kushuhudia utajiri wa historia ya kipekee inayopatikana lamu hata hivyo juhudi zaidi zinahitajika hasa kutoka kwa wizara ya utalii kuboresha sekta hii adhimu.
Ili kaunti ya lamu iendelee kunawiri na kuwa kivutio cha kipekee cha utalii juhudi zaidi zinahitajika kuboreshq sekta hii na si kutegemea vivutio asili pekee kama vile fukwe za bahari na mji wa kale.
Wizara ya utalii na utamaduni inatengewa fedha kila mwaka wa kifedha ila wakaazi wa lamu wanalalamika kuwa hawaoni fedha hizo zinapokwenda kwani sekta hiyo hawajabuni kitu chochote kuvutia watalii nje ya vivutio halisia vilivyopo.
Kudorora kwa sekta ya utalii kutapelekea kupungua kwa ajira na bila shaka kuboreka kwa sekta hiyo ni kuongeza nafasi za ajira na kuinua hali za kiuchumi za wakaazi wa lamu. Katika kaunti ya lamu watu wengi wanajipatia riziki kupitia hoteli, boti biashara za sanaa na huduma za watalii hivyo basi ipo haja ya ubunifu zaidi kuboresha sekta hii muhimu.
Serikali ya kaunti pia itaongeza mapato ya ushuru kutokana na shughuli za kitalii kwani ndio vitega uchumi vikubwa na tegemewa lamu hivyo basi inashangaza kuona juhudi zaidi hazionekani kuboresha kitengo hichi muhimu.
Sekta ya utalii ndio uti wa mgongo wa uchumi wa lamu na ni chanzo kikuu cha ajira na maendeleo ya jamii. Sekta hii si tu injini ya kiuchumi bali pia ni nguzo ya kijamii na kitamaduni. Inalisha familia, inalinda historia na mazingira na kuipa kaunti ya lamu nafasi ya kipekee ulimwenguni. Kuikuza na kuilinda sekta hii ni kuhakikisha kuwa urithi wa lamu unaendelea kung’aa kwa vizazi vijavyo na kuendelea kuvutia dunia nzima.